BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
TIMU ya Yanga imeanza vema kuutumia uwanja wa Uhuru uliopo jijini Dar es Salaam baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Majimaji katika muendelezo wa ligi kuu ya Vodacom.

Yanga walianza kwa kasi mchezo huo ambapo dakika ya 16 walipata penalti kufutia kiungo wa Majimaji Alex Kondo kuunawa mpira kwenye eneo la hatari.

Penalti hiyo ilizua sintofahamu kwa wachezaji wa Yanga na mashabiki baada ya kurudiwa mara tatu kutokana na mpigaji Simon Msuva kukosea. Kiungo Deus Kaseke aliwapatia mabingwa hao goli la uongozi baada ya kupokea krosi ya Amissi Tambwe aliyeunasa mpira wa penalti ya tatu uliogonga mwamba.

Licha ya Yanga kutawala sehemu kubwa ya mchezo huo lakini Majimaji walikuwa wajanja kwa kukaba kuanzia eneo la katikati ya uwanja na kuwanyima nafasi vijana hao Jangwani.

Majimaji walicheza kwa utulivu zaidi kipindi cha pili lakini walikosa ubunifu wa kupenya kwenye safu ya ulinzi ya Yanga iliyokuwa chini ya nahodha Nadir Haroub na Andrew Vicent 'Dante'.

Tambwe aliipatia Yanga goli la pili dakika ya 79 baada ya kupokea mpira wa krosi uliopigwa na Msuva upande wa kulia na kumuacha mlinda mlango Agathon Anthony akiwa hana la kufanya.

Dakika tano baadae Tambwe tena aliipatia Yanga goli la tatu akimalizia kwa shuti kali krosi iliyopigwa kwa ustadi na winga Juma Mahadhi.

Yanga iliwatoa Obrey Chirwa, Dante na Msuva nafasi zao zikachukuliwa na Mahadhi, Kelvin Yondani pamoja na Yusuph Mhilu. Kwa upande wa Majimaji walimpumzisha Paulo Mashona na kumuingiza Peter Mapunda.

Post a Comment

 
Top