BOIPLUS SPORTS BLOG

Karim Boimanda
MECHI ya watani ina mambo jamani. Kama ulidhani burudani yake ni ndani ya dakika 90 tu basi unajidanganya, burudani ya mtanange huu huanzia katika maandalizi.

Baada ya kupoteza mchezo wake dhidi ya Stand United huko Shinyanga, Yanga ilikwea 'pipa' hadi Pemba ambako wameweka kambi maalumu kwa ajili ya mchezo wa ligi kuu dhidi ya Wekundu wa Msimbazi Simba.

Unajua hali ikoje huko Pemba?, jamaa wamefunga 'vioo', si mwandishi wa habari wala shabiki ambaye anaruhusiwa kutia maguu kirahisi kambini hapo.

Sasa sikia kilichotokea upande wa pili kwa Wekundu wa Msimbazi. Baada ya jana kusambaa picha na video mbalimbali zikiwaonyesha wachezaji wa Simba wakiwa mazoezini kambini kwao mjini Morogoro, vigogo wa timu hiyo walikaa wakatafakari, wakasema "msitutanie, kuanzia leo hakuna mtu kusogelea kambi hiyo." 

 BOIPLUS inafahamu kuwa vigogo wa wekundu hao walishtushwa na kitendo cha picha hizo kusambaa mitandaoni ndipo walipoamua kufunga 'mageti' kabisa.

Simba na Yanga zitavaana jumamosi hii katika mchezo wa ligi kuu ya Vodacom huku Simba ikiongoza ligi kwa pointi 16 na Yanga ikishika nafasi ya tatu na pointi zao 10 lakini ikiwa na mchezo mmoja mkononi.

Post a Comment

 
Top