BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi wetu
BEKI wa kati wa timu ya Yanga Kelvin Yondani ameenguliwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa kilichosafiri leo hii kwenda Nigeria kwa ajili ya mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi kuwania nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2017.

Taarifa ambazo Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imezipata ni kwamba Yondani ana matatizo ya kifamilia ambayo hajayaweka sawa hadi timu hiyo inaondoka kwenda Nigeria na Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa hajajaza nafasi hiyo.

Mkwasa amekerwa na kitendo hicho, lakini TFF itasubiri ripoti ya kocha huyo mara baada ya kurejea kutoka Nigeria.

Timu hiyo imeondoka na wachezaji 18 huku ikitarajiwa kuungana na na Nahodha wa timu hiyo, Mbwana Samatta nchini Nigeria. 

Mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania anayechezea timu ya KRC Genk ya Ubelgiji anatokea jijini Brussels ambako makocha wake wamewaomba Mkwasa na Daktari wa Taifa Stars, Richard Yomba kuangalia namna ya kumtumia kwa sababu ana uchovu wa mechi ngumu zilizoipa matokeo mazuri ya kutinga hatua ya makundi ya ligi ya Europa.

Taifa Stars inakwenda Nigeria kwa ajili ya mchezo huo dhidi ya timu ya taifa ya nchi hiyo, Super Eagles utakaofanyika Septemba 3.

Licha ya mchezo huo kuwa sehemu ya mchuano wa kuwania nafasi ya kucheza fainali hizo za AFCON 2017 huko nchini Gabon, lakini utakuwa ni wa kukamilisha ratiba tu baada ya Misri kufuzu kwa fainali hizo kutoka kundi G ambalo mbali ya Nigeria na Tanzania, pia ilikuwako Chad ambayo iliyojitoa katikati ya mashindano.

Post a Comment

 
Top