BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
Afande Sele akisaini mkataba wa kutumbuiza kwenye tamasha la muziki wa taarabu

MSANII nguli wa muziki wa kizazi kipya Selemani Msindi 'Afande Sele' amesaini mkataba wa kutumbuiza kwenye Tamasha la Muziki wa Taarabu 'Nani Zaidi' litakalofanyika Desemba 25 katika Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.

Tamasha hilo pia litawashindanisha Wasanii nguli wa mziki wa taarabu ambao ni Mwanahawa Ally, Hadija Kopa pamoja na Hadija Yusuph ambao wote wamethibitisha kushiriki baada ya kusaini mkataba.

Tamasha hilo linaloratibiwa na Mtandao wa Habari wa vijana Tegemeo Arts Group Tanzania (TAGT) lina dhamira ya kuhamisisha watu kujitolea damu kwa ajili ya kuokoa maisha ya wale wenye shida na kusambazwa kwenye hospitali mbali mbali mkoani Morogoro.

Akizungumza baada ya kusaini mkataba huo Afande Sele alisema amehamasika kushiriki tamasha hilo kwakua suala la damu kwenye mkoa huo ni changamoto huku ajali nyingi zinazohitaji damu zikitokea na kulazimika kuazima jijini Dar es Salaam.

"Mkoa wa Morogoro unaunganisha mikoa mbali mbali nchini na ajali nyingi hutokea hivyo suala la damu ni jambo ambalo haliwezi kuepukika. Kama unakumbuka Mbaraka Mwishehe alikufa kwa ajali lakini kama damu ingepatikana kwa haraka basi tungeweza kuokoa maisha yake," alisema Afande.
Meneja wa FM Academia, Kelvin Milinga kulia akisaini mkataba

Bendi ya FM Academia nayo imethibitisha kushiriki tamasha hilo baada ya Meneja wake Kelvin Milinga kusaini mkataba na kukabidhiwa hundi kama malipo ya awali ya ushiriki.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa TAGT Hamisi Abdallah 'Kajumulo' alisema sehemu ya mapato yatakayo patikana kwenye Tamasha hilo yatatumika kuwanunulia wanafunzi 100 wenye mazingira magumu vifaa vya shule kutoka mikoa mbali mbali nchini ikiwemo visiwani Zanzibar.

Post a Comment

 
Top