BOIPLUS SPORTS BLOG

Zainabu Rajabu,Chamazi
TIMU ya Azam imelazimishwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Maafande wa  Ruvu Shooting katika mchezo wa ligi kuu Tanzania Bara uliochezwa kwenye uwanja wa Azam Complex uliopo nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam. 

Mchezo huo ulianza kwa kasi ambapo  Azam walilishambulia  lango la Ruvu lakini katika dakika ya tisa mshambuliaji Fully Maganga aliwashangaza Azam kwa kuiandikia Ruvu goli la kuongoza akimchambua kipa Aishi Manula.

Azam waliendelea kuliandama lango la Maafande hao ambapo dakika ya 30 Hamisi Mcha alipiga mpira wa kona uliounganishwa kwa kichwa na kiungo Jean Mugiraneza na kuisawazishia Azam.

Mcha aliiwapatia wenyeji goli la pili dakika ya 69 baada wachezaji wa Maafande hao kufanya mzaha kwenye lango lao kabla ya winga huyo kufunga kwa shuti kali.

Kiungo mkongwe Shaban Kisiga 'Malon' aliwasawazishia wageni dakika ya 89 kwa shuti kali baada ya mabeki wa Azam kujisahau kuondoa hatari langoni mwao.

Azam iliwatoa Mudathir Yahya na Hamis Mcha na nafasi zao zikachukulia na Frank Domayo pamoja na Ramadhani Singano huku wa Ruvu  ikiwatoa Said Dilunga, Yusuph Nguya, JabirAziz na  kuwaingiza na  Ayoub kitala, Chonde Magonja,  Baraka Mtuwi.

Post a Comment

 
Top