BOIPLUS SPORTS BLOG

Zainabu Rajabu, Chamazi
HALI imezidi kuwa mbaya kwa timu ya Azam FC baada ya leo tena kulazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Azam Complex uliopo nje kidogo ya jiji  la Dar es Salaam.

Azam chini ya Kocha Mhispania Zeben Hernandez imekuwa haipati matokeo mazuri baada ya kushinda michezo mitatu, kutoka sare mitatu na kupoteza mitatu ambapo hata Wachezaji wa 'Wanalambalamba' hao wanaonekana kukosa moyo wa kupambana kama ilivyokuwa msimu uliopita walipomaliza ligi wakiwa nafasi ya pili.

Mshambuliaji Rashidi Mandawa aliipatia Mtibwa bao la uongozi dakika ya pili ya mchezo kwa kichwa baada ya kumalizia mpira mrefu wa krosi uliopigwa na beki wa kulia Ally Shomari kabla ya Himid Mao kusawazisha dakika ya 11 kwa mkwaju wa penalti.


Mchezo huo ulikuwa wa kasi kiasi huku timu zote zikishambuliana kwa zamu lakini umakini mdogo wa washambuliaji wa pande zote ulisababisha matokeo yabaki kuwa sare, endapo timu moja ingeongeza juhudi kidogo basi ingeweza kuibuka kidedea.

Hii ni mechi ya tatu mfululizo kwa Azam kushindwa kupata alama tatu baada ya kufungwa goli 1-0 dhidi ya Stand United ugenini na kutoka sare ya bila kufungana na Yanga kabla ya hii leo kukabwa koo na Mtibwa.

Matokeo hayo yanazidi kuweka rehani kibarua cha Kocha Hernandez kwakua inaonekana mabosi wa Azam wanaweza kushindwa kuvumilia kuona timu yao ikiendelea kushindwa kupata ushindi hata katika uwanja wake wa nyumbani waliouzoea.

Katika mchezo huo Azam iliwatoa Hamis Mcha, Jean Mugiraneza na Mudathir Yahaya na kuwaingiza John Bocco, Michael Bolou pamoja na Fransisco Zekumbawira. Kwa upande wa Mtibwa iliwapumzisha Mohamed Issa na kumuingiza Kasiani Ponela.

Post a Comment

 
Top