BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
AZAM FC yenye hasira ya matokeo inatarajia kuondoka kesho Jumatatu kuifuata Stand United kwa ajili ya mechi yao itakayochezwa Jumatano uwanja wa CCM Kambarage huku wakiwa na matumaini kibao ya kumaliza machungu ugenini.

Matajiri hao wa Ligi Kuu ya Vodacom wataondoka kwa ndege ya Shirika la Ndege la Precion mpaka Mwanza ambapo wataunganisha kwenda Shinyanga na baada ya mechi hiyo watalazimika kurudi jijini Dar es Salaam kutumia usafiri huo huo kuwahi maandalizi ya mechi yao dhidi ya Yanga itakayochezwa Jumapili ijayo.

Ofisa Habari wa Azam, Jaffar Idd alisema kuwa kutumia usafiri huo kwao ni jambo la kawaida ila awamu hii hawataki kuwachosha wachezaji wao kwani wanahitaji pia pointi tatu muhimu kutoka kwa Yanga huku wakiwa na kumbukumbu nzuri ya kuwafunga mabingwa hao kwa penalti kwenye mechi ya Ngao ya Hisani iliyomaliza kwa sare ya mabao 2-2 ndani ya dakika 90.

"Tunaondoka kesho Jumatatu, wachezaji watapumzika siku moja na baada ya mechi Alhamisi tutageuza Dar es Salaam tukiamini kwamba timu yetu itakuwa haijachoka na safari kuelekea mechi ya Yanga na wachezaji watakosafiri ni 19 tu," alisema Jaffar.

Azam bado haijawa na kasi yao ya msimu uliopita ambapo sasa inashika nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi kuu ikiwa na pointi 11 sawa na Yanga pamoja na Ndanda FC tofauti yao ni mabao ya kufunga na kufungwa huku Stand United iliyochini ya Mfaransa Patrick Liewig yenyewe inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 16 na tayari wamewatangazia vita wapinzani wao hao.

Post a Comment

 
Top