BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
TIMU za Azam na Yanga zimeshindwa kutambiana kwenye mchezo uliotawaliwa na fujo na kuondoa ladha ya mpira wote kiasi cha kusababisha mashabiki wao kuchukizwa na hilo.

Timu hizo zimetoka sare tasa katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru ambapo Azam wamezidi kuwa kwenye wakati mgumu baada ya kujikusanyia alama 12 kwenye michezo 9.

Mechi ilikuwa ya kukamiana zaidi ambapo wachezaji wa timu zote walichezeana rafu ambazo hazikuwa na umuhimu wowote lakini Mwamuzi Israel Nkongo alitumia busara kwa kutotoa kadi nyekundu.

Winga Simon Msuva alikuwa katika kiwango bora ambapo beki Erasto Nyoni alikuwa kwenye wakati mgumu sana upande wa kulia hadi ikafika hatua Daniel Amoah akawa anasaidia ili kupunguza kasi ya winga huyo.

Beki wa kulia wa Yanga Juma Abdul alishindwa kuendelea na mchezo baada ya kuumizwa na Amoah dakika ya 24 wakati akijaribu kushambulia kutoka pembeni sambamba na Msuva.

Kipindi cha pili Azam walimiliki zaidi mpira huku wakiwashambulia Yanga mara kwa mara lakini umakini mdogo wa washambuliaji wa Wanalambalamba hao uliwanyima mabao.

Nkongo aliwaonya kwa kuwaonesha kadi ya njano Erasto Nyoni, Mudathir Yahaya, na Francisco Zekumbariwa kwa upande wa Azam huku Donald Ngoma akionywa kwa upande wa Yanga.

Yanga iliwatoa Abdul, Deus Kaseke na Andrew na kuwaingiza Mbuyu Twite, Gofrey Mwashiuya na Nadir Haroub Canavaro huku Azam wakiwapumzisha Mudathir,John Bocco pamoja na Bruce Kangwa nafasi zao zikachukuliwa na Frank Domayo, Hamisi Mcha na Zekumbariwa.

Post a Comment

 
Top