BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
UONGOZI wa klabu ya Azam umekanusha vikali taarifa ya beki wake raia wa Ivory Coast Pascal Wawa kugoma kuwachezea 'Wana lambalamba' hao akishinikiza kuondoka kwenda kucheza soka la kimataifa.

Taarifa ambazo BOIPLUS ilizipata ni kwamba beki huyo kisiki aligoma kucheza katika mechi kadhaa zilizopita akitaka kuondoka kufuata nyayo za mchezaji mwenzake Kipre Tchetche aliyetimkia nchini Oman kabla ya kuanza kwa msimu huu.

Mkurugenzi Mkuu wa Azam Saad Kawemba alisema kuwa beki huyo  hajagoma kama watu wanavyotafsiri na kuhusu mchezaji anayetakiwa kucheza ni jukumu la kocha kupanga ila hali ya kikosi hicho ni shwari na hakuna tatizo na mchezaji yeyote.

"Mbona hata Agrey Morris hajacheza kwa muda mrefu watu hawasemi, nikwamba hakuna mgomo wowote kwa mchezaji yoyote ndani ya timu ya Azam," alisema Kawemba.

Azam juzi walilazimishwa sare ya mabao 2-2 na Maafande wa Ruvu Shooting nyumbani na kuwatupa hadi nafasi ya sita katika msimamo wa ligi kuu baada ya kujikusanyia alama 11 pekee mpaka sasa.

Baada ya mapumziko ya mechi za kimataifa Azam watasafiri kuelekea mkoani Shinyanga kucheza na Mwadui FC katika mechi ya mzunguko wa nane.

Post a Comment

 
Top