BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi wetu
Kocha Rogasian Kaijage

BAADA ya Kocha wa Mwadui FC Jamhuri Kihwelo 'Julio' kutangaza kuachana na soka kwa madai ya uamuzi mbovu wa marefa, naye Kocha Mkuu wa Toto Africans Rogasian Kaijage ameamua kujiweka pembeni kwa madai ya kwamba kuna kundi la watu ndani ya timu hiyo wanamuingilia kwenye majukumu yake.

Hatua hiyo imekuja baada ya kichapo cha jana cha bao 1-0 dhidi ya Ndanda ambapo baadhi ya mashabiki wa timu hiyo walimzonga kocha huyo wakitaka kumpiga hadi aliposaidiwa na Jeshi la Polisi lililowahi na kuwatawanya kabla hali hajawa mbaya zaidi.

Kaijage alisema kuwa aliamua kujitolea kuisaidia timu hiyo lakini Uongozi wa 'Wanakishamapnda' umeshindwa kuwadhibiti wanachama hadi wanamuingilia kwenye majukumu yake hali iliyomfanya kuamua kujiweka pembeni.

"Siwezi kufanya kazi katika mazingira magumu kama haya nimeamua kurudi kwenye kazi yangu  ya kukuza vipaji vya soka kwa watoto na  tayari nimeshapanga na Halmashauri ya jiji la Mwanza kushirikiana kufanya kazi hiyo," alisema Kaijage.

Toto wanashika nafasi ya 14 kwenye msimamo wa ligi kuu baada ya kujikusanyia alama tano zilizotokana na kushuka dimbani mara saba.

Post a Comment

 
Top