BOIPLUS SPORTS BLOG Karim Boimanda
LEO mzee wa Black & White nimeamka na kumbukumbu ya kutisha kidogo, enzi hizo baada ya kumaliza shule halafu mtu hutaki kubanwabanwa 'home', unaamua kujichanganya na 'wana' gheto ambako hupangiwi muda wa kulala wala kuamka, ila sheria ngumu ni 'Akachangile akadundi'.

Naamini watoto wa kitaa wamenisoma, hapo namaanisha 'Asiyechangia hali'. Maisha yalikuwa ni kuchanga tu, ukifika muda wa kula wanaopiga tonge ni wale tu waliochangia mlo huo, kama hujachanga utaishia kutazama tu mwanangu.

Achana na hayo bwana, hebu turejee kwenye mchezo unaotusahaulisha matatizo yetu mida mingine, soka. Huku si unajua hata kama mtu anakudai, akipiga simu wakati upo uwanjani pale unamwambia 'Nipigie baadaye kidogo mwanangu kuna kelele". Hapo angalau unapata masaa mawili ya kujipanga umwambie nini akipiga tena.

Nakumbuka wababe wa kitaa cha Msimbazi walihangaika kama misimu miwili hivi kumfukuzia mchawi wa mabao wa Vital'O ya Burundi, Laudit Mavugo. Unadhani viongozi wa Simba ni wehu?, aah wapi, waliona kitu, jamaa analijua goli bwana, kwa misimu miwili mfululizo kwenye  ligi ya Burundi aliibuka mfungaji bora tena akiwa amepachika jumla ya mabao yasiyopungua 60.

Msimu huu wakamtia mikononi awafanyie kazi, kwa mkwara tu mechi yake ya kwanza ya kirafiki akaweka moja huku akihusika katika upatikanaji wa mabao mengine mawili pale kwa Mchina (Uwanja wa Taifa), watu Oyooooo!. Mzee wa Black & White nikamchekiii nikaona humu mchezaji yumo, bila kupepesa macho wala ulimi.Ligi ilianza Mnyama akivaana na Ndanda FC, Mavugo alitupia kama kawa, ungewaambia nini tena hapo Lunyasi kuhusu Mavugo wao wakuelewe?. Matarajio yote wakayahamishia kwa straika huyo ambaye akipiga mpira ukakukuta ukiwa na afya nusu kilo basi tunaweza kuzungumza mengine kama watachelewa kukukimbiza hospitali.

Mavugo akajua kuwa yeye ndiye tegemeo, kwa nia njema tu akatia nia kuwa kila 'game' lazima ampeleke kipa kwenye nyavu, hapo sasa ndipo mambo yalipobadilika, ikawa hata akishuka kusaidia mabeki, akiupata tu mpira basi mwanetu anawaza kutupia bila kujali yuko wapi.

Hadi sasa sijaona straika anayetengeneza nafasi nyingi uwanjani kama Mavugo, mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni, jamaa anajua kuwakimbia mabeki, mfuatilie michezo miwili tu utazame pasi anazopewa zinamkuta akiwa katika mazingira gani, utakubaliana na mimi. Ni ngumu sana kwa walinzi wetu hawa kumchunga Mavugo kila wakati.

Joseph Omog hapa ana mgodi, labda tu bado hajajua jinsi ya kuutumia. Kila kocha anatamani kuwa na mchezaji mwenye uwezo mkubwa wa kutengeneza nafasi kama alivyo Mavugo, halafu baada ya hapo anamtengeneza kuwa mpishi mzuri. Mavugo abadilishiwe tu majukumu, jina lake litaimbwa hadi kwenye Singeli.

Kwani unadhani shida ya Mavugo ni nini?, si kutaka kufunga tu?. Anasahau kuwa 'mchongo' wa kwanza ni timu kupata ushindi kabla hajajifikiria yeye mwenyewe. Nafasi anazopata akiwa ndani ya 18 hasa eneo la kushoto, kama zote angekuwa anapiga krosi kuingia ndani basi leo tungekuwa tunamtaja kama mchezaji aliyechangia upatikanaji wa mabao mengi zaidi katika ligi kuu.Nilikuwa natazama mabao manne aliyofunga hadi sasa, mawili ni ambayo kama angekosa bado angeitwa mchoyo. Ni kama vile alifanya majaribio yake yale yale ambayo mara nyingi amekuwa akikosea na kuinyima timu mabao.

Sasa naona mshua kaamua kuanza kumpiga benchi na akimuanzisha basi akizingua tu hajiulizi mara mbili, anamuita wapige stori pale nje huku mechi inaendelea. Kiroho safi tu huu bado si msaada kwa Mavugo, njia pekee ya kumsaidia nyota huyo ni kumpeleka kwenye maisha ya Gheto, Akachangile Akadundi.

Mavugo achanwe 'live', kuanzia sasa hakuna kula kabla hujachangia. Kabla hajawaza kufunga basi awaze kwanza kutengeneza mabao angalau matatu. Alazimishwe kuishi maisha ya kusubiri mabao yamfuate, asiyafuate tena. Mimi naamini akitoa pasi za mabao katika mechi tatu mfululizo atarudi kuwa Mavugo yule wa Vital'O.

Hii ni kwasababu wale atakaokuwa anawapa pasi nzuri zitakazowawezesha kufunga mabao laini ndio hao hao watakaokuwa wakimtafuta akiwa katika maeneo mazuri na kumpa pasi atupie. Akachangile Akadundi babu, vinginevyo muda si mrefu tutasikia 'single' mpya.

 Mobile; +255788334467
 E-Mail; karim@boiplusmedia.com

Post a Comment

 
Top