BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi Wetu, Mbeya
Kocha wa Mwadui, Jamhuri Kihwelu 'Julio' ameachana rasmi kufundisha soka la Bongo huku sababu kubwa ikiwa ni waamuzi kutochezesha kwa kufuata sheria 17 za soka. 

Julio amekumbusha hata bao la Amissi Tambwe kuwa mwamuzi hakuwa sahihi kukubali bao hilo linalodaiwa kufungwa baada ya mshambuliaji huyo kumili mpira kwa mkono hivyo haoni sababu za kuendelea kuwa tena kocha wa mpira Tanzania.

"Matatizo yote haya tunalalamika ila tunakuwa kama tunatwanga maji kwenye kinu hivyo kuanzia sasa nimeacha kuwa kocha wa soka hapa Tanzania, kama nitafurahi nitakwenda kuangalia mpira na si kinyume cha hapo acha nipumzike nifanye shughuli zangu.

"Siondoki kwa sababu ya kufungwa ila napoteza muda mwingi, naacha familia yangu, nilianza kuongea toka mechi ya Kagera Sugar ila nilionekana najitetea leo tumenyimwa penati  ya wazi, imeniuma sana mpira unakokwenda siko ila ngoja nipumzike kuliko kupoteza muda wangu," alisema Julio.

Julio alisema uamuzi wake si kwamba ametumia hasira ila ni vitu ambavyo vinamuumiza hivyo mpira kwake hauna faida.

"Na tulitaarifiwa mapema kabla ya mechi kuwa lazima tutafungwa, sikatai kufungwa na bao lao ni zuri tu, ila tunatumia muda mwingi lakini bado tunanyimwa haki yetu, sitaki tena mpira na nitaenda kwenye ufukwe wa Coco kula mishikaki kama sitajisikia kwenda uwanjani kuangalia mechi," alisema Julio ambaye timu yake leo imepoteza mechi dhidi ya Mbeya City kwa bao 1-0

Post a Comment

 
Top