BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
WINGA wa Mtibwa Sugar, Haruna Chanongo sasa amezaliwa upya na kusisitiza kuwa ubora wake utazidi kuonekana kadri siku zinavyokwenda kwani maisha aliyojifunza chini ya Patrick Liewig akiwa Stand United yamebadilisha na sasa anapambana upya.

Alipokuwa Stand United, Chanongo alitibuana na Mfaransa Liewig kwa madai ya utovu wa nidhamu alipokwenda kufanya majaribio TP Mazambe bila ruhusa ya kocha huyo mwenye misimamo na kazi yake na hivyo alianza kukalia benchi kutoka kikosi cha kwanza.

Msimu huu Chanongo amesajiliwa Mtibwa Sugar na tayari ametikisa nyavu mara tatu huku akiweka wazi maisha ya Mtibwa kwamba mchezaji anayejituma ndiye anapata nafasi kwani kocha Salum Mayanga haangalii sura ama urafiki wa mchezaji.

Akizungumza na BOIPLUS Chanongo alisema kuwa; "Maisha yanabadilika na ninapaswa kupambana kurudi kwenye kiwango changu cha zamani, nashukuru nipo Mtibwa najifunza mambo mengi ambayo yananisaidia kunitengeneza kisoka tofauti na nilipokuwa Stand wakati wa Liewig japokuwa maisha yale nayo yalinifundisha.

"Binafsi naamini nitarudi kwenye ubora wangu, nafurahishwa na jinsi kocha wetu ambavyo hana upendeleo wa kuwatumia wachezaji anaowapenda, pale ukijituma basi unapata nafasi na ni jambo ambalo kocha anasisitiza kila mara, kujituma na kujitambua, hivyo ukiwa Mtibwa lazima utambue hayo mambo, hakuna starehe zaidi ya kazi, unaenda mazoezi unarudi kulala pamoja na mechi tu," alisema Chanongo.

Tangu ajiunge na Mtibwa Sugar, kiungo huyo ambaye ni zao la Simba amekuwa kwenye kikosi cha kwanza cha Mayanga huku ubora wake ukianza kuonekana ingawa yeye amasema safari yake haijaishia hapo ndio maana ameamua kupambana kwa nguvu zote.

Post a Comment

 
Top