BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
MSHAMBULIAJI Obrey Chirwa ametoa 'gundu' baada ya kufunga bao lake la kwanza tangu asajiliwe na mabingwa hao katika ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Mtibwa Sugar katika muendelezo wa ligi kuu ya Vodacom mchezo uliofanyika kwenye uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Mchezo huo ulianza kwa kasi huku timu zote zikishambuliana kwa zamu lakini Yanga ndiyo walifika zaidi langoni mwa Mtibwa ila ulinzi uliowekwa na mabeki Kasiani Ponela na Dickson Daudi ulikuwa kikwazo.

Kiungo Deus Kaseke hakuwa katika ubora wake katika mechi ya leo kutokana na kupoteza pasi nyingi huku baadhi akizirudisha nyuma na kupunguza mashambulizi kwa upande wa mabingwa hao mpaka Kocha Hans Pluijm alipomtoa dakika ya 45.

Chirwa aliipatia Yanga bao la kwanza dakika ya 45 baada ya krosi ya Simon Msuva kuokolewa vibaya na mabeki wa Mtibwa kabla haujamkuta straika huyo aliyetabiriwa kuibeba Yanga katika makala iliyowekwa kwenye mtandao huu mapema leo.

Dakika ya 63 Haruna Chanongo aliisawazishia Mtibwa kwa shuti kali ndani ya eneo la hatari baada ya mawasiliano hafifu baina ya mlinda mlango Deo Munishi na mabeki wake.

Dakika tano baadae Msuva aliipatia Yanga goli la pili kwa shuti kali baada ya kufanya shambulizi la haraka kutoka katikati ya Uwanja ambapo wachezaji wa Mtibwa hawakuwa na la kufanya.

Donald Ngoma aliipatia Yanga bao la tatu dakika ya 80 akimalizia krosi safi toka kwa Geofrey Mwashiuya upande wa kushoto baada ya kumuacha beki wa kulia Rogers Gabriel.

Yanga iliwatoa Kaseke, Chirwa na Saidi Makapu nafasi zao zikachukuliwa na Mwashiuya, Mbuyu Twite na Ngoma. Mtibwa iliwapumzisha Ibrahim Jeba, Chanongo na Mandawa na kuwaingiza Stamili Mbonde, Hussein Javu pamoja na Kelvin Friday.

Post a Comment

 
Top