BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
KAMATI ya masaa 72 ya Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) itakutana kesho asubuhi kujadili vurugu zilizojitokeza kwenye mchezo wa ligi daraja la kwanza kati ya Coastal Union na Timu ya Manispaa ya Kinondoni (KMC) uliofanyika kwenye Uwanja wa CCM Mkwakwani jijini Tanga.

Mchezo huo uliochezeshwa na Mwamuzi Thomas Mkombozi ulimazilika kwa wenyeji Coastal kukubali kichapo cha mabao 3-2 ambapo mashabiki wa Wagosi hao walimshushia kipigo kikali refa huyo baada ya kumalizika kwa mchezo kutokana na kutoridhishwa na maamuzi yake huku wakidai kuwa ndiye chanzo cha timu yao kufungwa.

Afisa Habari wa TFF Alfred Lucas alisema Kamati hiyo imechelewa kuketi kwavile ripoti ya mwamuzi, Kamisaa wa Mchezo pamoja na Chama cha soka mkoa wa Tanga zilichelewa kuwafikia lakini kesho ndiyo siku ya hukumu.

"Kamati itaketi kesho asubuhi na tunategemea mpaka mchana hukumu itatolewa ili haki iweze kufuatwa kwa atakayebainika hakufuata sheria," alisema Lucas.

Endapo Coastal itakutwa na hatia inaweza kupata adhabu moja kati ya kucheza Uwanjani hapo bila mashabiki au kuhamishwa kituo ili kukomesha vitendo hivyo visivyo vya kiungwana michezoni.


Post a Comment

 
Top