BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
KATIBU mkuu wa Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) Celestine Mwesigwa amefungua kozi ya Wakufunzi ya waamuzi itakayokuwa na washiriki 32 kutoka nchi za Afrika zinazozungumza Kiingereza itakayodumu kwa siku tano.

Katika kozi hiyo Tanzania itawakilishwa na watu sita ambao wanne watakuwa kwenye masuala ya Ufundi huku wawili wakiwa kwenye utimilifu wa viungo. Washiriki hao ni Israel Nkongo, Josephat Bulali, Charles Mchawe, Alfred Lwiza, Soud Abdi, Pascal na Chiganga.

Mwesigwa alisema kuwa katika mpira wa miguu eneo la uamuzi ndilo lina changamoto kubwa ambalo limekuwa likilalamikiwa na wadau wengi wa soka kote ulimwenguni na ndiyo sababu FIFA wamekuwa na utaratibu wa kuanzisha kozi hizo ambazo ni mara ya tatu kufanyika nchini ndani ya miaka mitatu.

"Sheria za soka zimebadilika sana kwahiyo waamuzi wanatakiwa kupata kozi mbali mbali ili waendane na kasi ya mabadiliko hayo ili kuepuka malalamiko kutoka kwa wadau ambayo yanaweza kuepukika," alisema Mwesigwa.

Nae Kaimu Kiongozi Mkufunzi wa Waamuzi kutoka FIFA Manuel Navaro alisema kozi hiyo itakuwa msaada mkubwa kwa waamuzi kutoka barani Afrika kujua sheria mpya za soka na falsafa zake ili kuondoa malalamiko ambayo wakati mwingine husababisha vurugu zinazopelekea watu kujeruhiwa au kupoteza maisha kabisa.

Mmoja wa Wakufunzi kutoka Tanzania, Nkongo alisema kozi hiyo itawasaidia kuzifahamu sheria hizo mpya na kuwafundisha waamuzi wengine wa hapa nchini ili haki ifuatwe ambapo kila mtu atapata kinachostahili na kuondoa kabisa malalamiko.

Post a Comment

 
Top