BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
FRIENDS Rangers ni kama 'imeokota dodo' chini ya mpera baada ya kuzindukia mikononi mwa Ashanti United kwani ilikuwa imeanza vibaya ligi kwa kipigo pamoja na sare.

Mechi yao ya kwanza ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL), Rangers ilipigwa bao 5-0 na Mshikamano halafu ikatoka sare tasa na Pamba na leo imepata pointi tatu kwa kuifunga Ashanti bao 1-0, mechi hiyo imechezwa uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam.

Katika pambano hilo lililokuwa na ushindani mkubwa ambalo mashabiki wa pande zote mbili walijitokeza kwa wingi lakini wachezaji wa timu hizo walionekana kucheza bila malengo.

Kiungo Yusuph Fabo ndiye aliyeipatia Rangers bao pekee dakika ya 10 kwa shuti kali katikati ya uwanja lililogonga mwamba wa juu na kuingia wavuni hali iliyoamsha shangwe za mashabiki wa timu hiyo yenye makao makuu yake Magomeni Kagera.

Licha ya kuwa nyuma kwa bao moja lakini Ashanti waliendelea kulisakama lango la Rangers ambapo Yahaya Zayeed alikosa mkwaju wa penalti dakika ya 65 baada ya mlinzi mmoja wa Rangers kuunawa mpira kwenye eneo la hatari.

Mechi nyingine iliyofanyika uwanja wa Mabatini Mlandizi mkoani Pwani timu ya Manispaa ya Kinondoni (KMC) imeibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mbeya Kwanza ya jijini Mbeya. Mabao yote mawili yakiwekwa nyavuni na straika Rashid Roshwa.

Post a Comment

 
Top