BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
BAADA ya kukubali kichapo cha bao 1-0 kwenye Uwanja wa Mabatini Mlandizi mkoani Pwani toka kwa Maafande wa Ruvu Shooting Kocha wa timu ya Mbeya City Kinnah Phiri amehamisha hasira zake kwa Ndanda FC mchezo utakaofanyika kesho.

City wamesafiri hadi mkoani Mtwara tayari kwa mchezo huo utakaofanyika kesho kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona huku wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza mechi ugenini hali inayowapa chachu ya kutafuta ushindi kwa namna yoyote kuwatuliza mashabiki wao.

Phiri raia wa Zambia alisema safu yake ya kiungo ndiyo ilisababisha kupoteza mchezo dhidi ya Maafande hao na walikuwa na uwezo wa kusawazisha bao  lakini mwamuzi hakuwa upande wao na aliwanyima penati ya wazi ambayo ingeweza kusaidia kupata sare.

"Timu ipo vizuri wachezaji wote wana morali ya juu kuhakikisha tunafanya vyema kwenye uwanja wa ugenini japokuwa sio rahisi sana lakini tumejipanga kuondoka na alama zote," alisema Phiri.

Wagonga Nyundo hao wa jiji la Mbeya hawako katika kiwango bora kiuchezaji kama ilivyokuwa misimu miwili iliyopita kutokana na kushindwa kupata matokeo mazuri  baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo dhidi ya Simba(0-2) na Ruvu Shooting(1-0) hali ambayo inawatia shaka mashabiki wa timu hiyo.

City inashika nafasi ya 9 kwenye msimamo wa ligi baada ya kujikusanyia alama 12 kutokana na michezo 10 iliyoshuka dimbani hadi sasa huku Mzambia huyo akiwataka mashabiki wa timu kutokata tamaa kwakua ligi bado ni mbichi.

Post a Comment

 
Top