BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
Salum Mayanga, kocha Mtibwa Sugar
 UONGOZI wa Mwadui FC upo katika mazungumzo ya siri na kocha wa Mtibwa Sugar, Salum Mayanga ili kurithi mikoba ya Jamhuri Kihwelu 'Julio' ambaye amejiuzuru kufundisha soka la Tanzania kwa madai ya kuwa waamuzi wanatoa uamuzi mbovu kwenye mechi za ligi.

Habari za ndani kutoka Mwadui zinasema kuwa tayari mazungumzo ya awali yamefikia patamu na kocha huyo mwenye leseni A, hivyo kuna kila dalili kwamba huenda Mayanga akaachana na Mtibwa Sugar aliyoanza kuifundisha msimu huu akitokea Prisons.

Mayanga amepokea mikoba ya Mecky Mexime aliyekwenda Kagera Sugar, hivyo kama Mayanga ataamua kuondoka basi Mtibwa Sugar itapata changamoto mpya ya kusaka kocha mwingine kwa kipindi hiki ama wakati wa mapumziko mafupi ya ligi kuu.

Hata hivyo, Katibu Mkuu, Ramadhan Kilao hakutaka kuthibitisha hilo moja kwa moja ingawa habari zilieleza kuwa Mayanga ameonyesha nia ya kuwakubalia wachimba madini hao wa Shinyanga kwani mkataba wake na Mtibwa Sugar haumbani.

Kilao alisema kuwa jana walikuwa na kikao cha kujadili barua iliyowasilishwa na Julio ambapo wamebariki uamuzi wake na pia wameanza kupokea maombi mbalimbali kutoka kwa makocha wazawa na wageni ila wao hawapo tayari kuwa na kocha wa kigeni hivyo kwa asilimia kubwa kocha mgeni anayetajwa kuwa ni raia wa Burundi na yule wa Kenya, Yusuph Chipo maombi yao yanaweza kupigwa chini kabla hata CV zao hazijapitiwa.

"Siwezi kusema nani atakuwa kocha wetu kwa sasa ila tumepokea simu nyingi kutoka kwa makocha mbalimbali, kwa kipindi hiki kila kocha atatajwa kuwa tunamchukuwa maana mchakato huo upo, ila tusubiri kwanza tukamilishe mchakato wetu, yupo kama Chipo, kuna simu imepigwa kutoka Burundi. Ukweli wa hili utajulikana hivi karibuni, Julio tumebariki maamuzi yake katika kikao chetu cha jana, hutuwezi kumlazimisha.

"Binafsi amesema atashirikiana na sisi katika kila jambo la kiufundi endapo tutahitaji ushauri wake, tunashukuru kuipandisha timu yetu, msimu uliopita alifanya vizuri na hata alipotufikisha sasa. Timu yetu ni nzuri na itaendelea kufanya vizuri," alisema Kilao.

Post a Comment

 
Top