BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi wetu
MLIMBWENDE Diana Edward Lukumay kutoka Kinondoni ameshinda taji la Miss Tanzania 2016 na kuwashinda warembo wengine 29 shindano lililofanyika kwa mara ya kwanza nje ya jiji la Dar es Salaam ambapo fainali hizo zilifanyika mkoani Mwanza usiku wa jana.

Mgeni rasmi kwenye mashindano hayo alikuwa Naibu Waziri Habari Sanaa Utamaduni na Michezo Anastasia Wambura ambaye aliwapongeza waandaji kwa ubunifu wao na kusaidia Watanzania kupata ajira.

Wambura amewata washiriki hao kuendelea kufanya kazi mbali mbali za kijamii kama walivyokuwa wakati wapo kwenye shindano ili Watanzania wanufaike na vipaji walivyobarikiwa na Mungu.

Mwenyekiti wa Kamati ya Miss Tanzania Hashimu Lundenga alisema mashindano hayo yatakuwa yakibadilika kila wakati kulingana na mazingira na kama yameweza kufanyika nje ya Dar es Salaam kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa miaka kadhaa iliyopita basi mikoa mingine nayo itapata nafasi kwa kuandaa fainali hizo miaka ijayo.

"Ubunifu unaendelea na tunategemea mwakani yatakuwa mazuri zaidi ya haya kikubwa ni sapoti kutoka kwa wadau mbali mbali," alisema Lundenga.

Nae mshindi wa taji hilo Diana alisema kinyang'anyiro kilikuwa kigumu hata wapinzani wake walikuwa bora sana ila anamshukuru Mungu kwa kupata nafasi ya kuwa Miss Tanzania mwaka 2016.

Miss Tanzania aliyemaliza muda wake Lilian Kamanzina aliwashukuru Watanzania wote kwa sapoti waliyokuwa wakimpa na amewataka waendelee kumuunga mkono Diana kama ilivyokuwa kwake.

Post a Comment

 
Top