BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
MSHAMBULIAJI wa Prisons, Jeremiah Juma ameanza mazoezi mepesi ya kuendesha baiskeli baada ya kukaa nje kwa kipindi kirefu kutokana na majeraha ya goti aliyoyapata wakati timu yake ikipambana na Mbeya City, mechi hiyo ilichezwa uwanja wa Sokoine jijini Mbeya huku daktari wa City, Dr Kaseko akifanya uungwana wa kumtibu.

Jeremiah aliumia goti baada ya kuangukiwa na beki wa City, Sankhani Mkandawile wakati wa purukushani za kuwania mpira na kusababisha kukosa mechi tano hadi sasa ingawa pia haijulikani lini daktari wake atamruhusu kufanya mazoezi kwa ajili ya mechi za ushindani.

Jeremiah alisema kuwa mazoezi yake ya kuzunguka na baiskeli yatakuwa ni ya siku moja tu na ndipo ataanza mazoezi mepesi kwa kufuata ratiba ya daktari wake ambaye ni daktari wa Mbeya City, Dr Kaseko.

 "Sasa hivi naendelea vizuri na leo nimefanya mazoezi ya kuendesha baiskeli kuzunguka uwanja mara tatu ni mazoezi ya siku moja na baadaye nitaanza mazoezi mepesi na timu, nashukuru Dr Kaseko kwa kunitibu na alipoondoka na timu kwenda Mtwara alinikabidhi kwa daktari mwenzake na wananitibu bure.

"Sio kwamba wananitibu kwasababu nimeumizwa na mchezaji wao bali naona ni moyo wa upendo tu walionao pamoja na uungwana tu, kwani mpira sio vita, nasikitika tu kukosa mechi nyingi ambapo napoteza malengo yangu ya ufungaji wa 
mabao mengi maana tayari nilifungua mlango wa mabao nilipofunga mechi yetu na Toto," alisema Jeremiah ambaye alikuwa mfungaji bora wa timu yao msimu uliopita akiwa na mabao 15.

Jeremiah alikosa mechi dhidi ya Mwadui, Kagera Sugar, JKT Ruvu, Mtibwa Sugar pamoja na hiyo ya jana ya Stand United na sasa itategemea na ripoti ya daktari juu ya maendeleo yake kama ataweza kucheza mechi zilizobaki kuelekea kwenye mapumziko mafupi. Prisons imebakiza mechi nne ambazo ni dhidi ya Mbao, African Lyon, Ndanda FC, Yanga na Simba.

Post a Comment

 
Top