BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
KWA mara nyingine winga Shiza Kichuya ameisaidia timu yake ya Simba kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar mchezo uliofanyika kwenye uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Hii ni mechi ya tatu mfululizo kwa Kichuya kufunga bao moja moja ambapo alifunga dhidi ya Yanga katika sare ya bao (1-1) Mbeya city (2-0) kabla ya leo kutupia jingine moja linalomfanya kufikisha mabao saba na kuwa kinara wa ufungaji wa ligi mpaka sasa.

Kama ilivyo kawaida ya Simba walimiliki sehemu kubwa ya mchezo huo ambapo Kagera walikuwa wakicheza nyuma na kufanya mashambulizi machache ya kushtukiza lakini umahiri wa safu ya ulinzi wa Wekundu hao uliokuwa chini ya Method Mwanjale na Juuko Murshid ulimzidi mbinu Danny Mrwanda aliyekuwa akiiongoza safu ya ushambuliaji ya  'Wanankulukumbi'.

Kiungo Muzamiru Yassin alifunga bao lake la kwanza kwa Wekundu hao tangu alipojiunga akitokea Mtibwa Sugar kwa kichwa dakika ya 44 kufuatia mpira wa kona iliyopigwa na Shiza Kichuya. 

Kichuya aliipatia Simba bao la pili kwa mkwaju wa penalti dakika ya 75 baada ya kiungo Mohamed Ibrahim kuangushwa kwenye eneo la hatari na mlinzi wa Kagera.

Mwamuzi Hussein Athumani kutoka mkoani Katavi aliwaonya kwa kuwaonesha kadi ya njano wachezaji Juuko Murshid, Muzamiru na Mwanjale kutokana na mchezo usio wa kiungwana waliounesha.

Simba iliwatoa Fedrick Blagnon, Ibrahim Ajib na Mwinyi Kazimoto na kuwaingiza Laudit Mavugo, Mohemedi pamoja na Saidi Ndemla. Kwa upande wa Kagera iliwatoa Mbaraka Abeid, Edward Christopher na Mrwanda nafasi zao zikachukuliwa na Ally Ramadhani, Paulo Ngwai pamoja na Themi Felix.

Post a Comment

 
Top