BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi Wetu
UONGOZI wa Klabu ya Kagera Sugar umewasimamisha wachezaji wao Hussein Sharif 'Casillas' ambaye ni mlinda mlango na beki Erick Charles kwa tuhuma za kuihujumu timu yao wakidaiwa kupanga matokeo katika mechi yao dhidi ya Yanga ambao waliibuka na ushindi wa mabao 6-2.

Mechi hiyo ilichezwa Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba ambapo Casillas alifungwa mabao matatu kipindi cha kwanza kabla ya kocha Mecky Mexime kufanya mabadiliko ya kumwingiza David Burhan ambaye pia alipigwa bao tatu.

Uongozi huo umewasimamisha wachezaji hao wawili kwa muda usiojulikana ili kupisha uchunguzi na endapo watakutwa na hatia basi watachukuliwa hatua za kisheria.

"Ni kweli wamesimamishwa. Sasa hivi wanafanya uchunguzi kwani hawana uhakika na jambo hilo kama kweli wamehusika katika mpango wa kupanga matokeo, ila wakikutwa na kosa hilo basi sheria zipo wazi hivyo tunasubiri kitakachotokea huko mbele," alisema mchezaji mmoja mkongwe wa Kagera.

Kagera wanaoshika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi kwa kujikusanyia alama 18 wanajiandaa na mechi yao dhidi ya Azam Fc itakayochezwa keshokutwa uwanja wa Kaitaba. Azam wenyewe wana pointi 16 tu wakiwa katika nafasi ya sita.

Post a Comment

 
Top