BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
KAMA ni mgeni hapa nchini isingekuwa rahisi kuamini kuwa timu unazotazama zikicheza ni za ligi kuu, labda mpira wa watoto huko mtaani maarufu kama 'chandimu'. Hiyo ni kutokana na kiwango duni kilichoonyeshwa katika mchezo wa ligi kuu kati ya African Lyon na Ndanda FC uliomalizika kwa wenyeji kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

Katika mchezo huo uliochezwa kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam wachezaji wa timu zote walionekana wakicheza kama wamelazishwa au wanaokabiliwa na uchovu wa hali ya juu jambo lililopelekea mechi kupoteza kabisa ladha.

Kama mwamuzi Selemani Kidugali angeamua kufuata ipasavyo sheria 17 za mchezo wa soka bila kuwa na huruma basi angeweza kuwatoa kwa kadi nyekundu wachezaji zaidi ya watatu kutokana na kucheza rafu ambazo hazikuwa na tija kulingana na mazingira na kuwafanya mashabiki wachache waliojitokeza uwanjani hapo kuishia kuduwaa.

Kiungo William Otong ndiye aliyefunga bao hilo pekee la Lyon dakika ya 76 baada ya kumalizia kwa kichwa krosi ya Omari Salum ambayo ingeweza kuokolewa na walinzi kutokana na kuonekana haina madhara.

Licha ya kufungwa bao hilo bado Ndanda walikuwa na nafasi ya kusawazisha lakini safu yao ya ushambuliaji iliyokuwa ikiongozwa na Omary Mponda haikuwa na ubunifu wa kupenya kwenye ngome ya Lyon.

Post a Comment

 
Top