BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Mbeya
MPACHIKA mabao wa Simba, Shiza Kichuya jana aliumia kifundo cha mguu na kushindwa kuendelea na mechi huku ikionekana kuwavuruga mashabiki wa timu hiyo lakini daktari Yassin Gembe amewatuliza kwa kuwaambia kuwa Kichuya atakuwa fiti na mechi ijayo huenda akacheza.

KIchuya aliumia baada ya kufanyiwa madhambi na mchezaji wa Mbeya City katika mechi ya jana iliyochezwa uwanja wa Sokoine ambapo Simba ilishinda bao 2-0 yaliyofungwa na Ibrahim Ajib na Kichuya, yote yalifungwa kipindi cha kwanza.

Akizungumza na BOIPLUS, Gembe alisema kuwa mpaka jana usiku winga huyo alikuwa anaendelea vizuri na kwamba huenda akacheza mechi yao ijayo dhidi ya Kagera Sugar itakayochezwa Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es salaam

"Jeraha lake si kubwa sana naamini mpaka Jumamosi atakuwa fiti, aliumia kifundo cha mguu na mpaka jana usiku alikuwa anaendelea vizuri," alisema Gembe.

Endapo Kichuya atakuwa hajakaa sawa basi kuna hatari ya kukosa mechi hiyo itakayochezwa Jumapili.

Post a Comment

 
Top