BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
DAKTARI wa timu ya Yanga Edward Bavu amewatoa hofu mashabiki wa timu hiyo kuhusu afya za nyota wao wawili waliopata maumivu kwenye mchezo uliomalizika kwa sare ya bila kufungana dhidi ya Azam katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam jana. 

Katika mchezo huo mabeki Juma Abdul na Vicent Andrew 'Dante' wakishindwa kuendelea na mechi baada ya kupata maumivu na kuzua taharuki miongoni mwa mashabiki wa mabingwa hao lakini Daktari huyo alisema nyota hao wanaendelea vizuri na muda si mrefu watarejea dimbani.

Bavu ameiambia BOIPLUS kuwa mabeki hao pamoja na mshambuliaji Amisi Tambwe watasafiri na timu hiyo kesho kuelekea jijini Mwanza  kwa ajili ya mchezo dhidi ya Toto african huku wakiendelea na matibabu kwakua hawakuumia sana.

"Tambwe yuko vizuri anaweza kutumika kwenye mechi dhidi ya Toto itategemea kocha kama ataona anafaa lakini Juma na Dante wao tutasafiri nao Mwanza kuendelea na matibabu ila kuhusu kama wataweza kushuka dimbani itafahamika kesho kwavile leo hakukuwa na mazoezi," alisema Bavu.

Tambwe ndiye kinara wa mabao wa mabingwa hao hadi sasa baada ya kucheka na nyavu mara nne katika michezo saba aliyoteremka dimbani huku Dante akiwa mhimili mkubwa kwenye safu ya ulinzi na tayari ameingia kikosi cha kwanza kutokana na umahiri wake hasa katika kucheza mipira ya juu licha ya kimo chake kifupi.

Bavu alisema mbali na wanandinga hao hakuna mchezaji mwingine majeruhi kwenye kikosi cha mabingwa hao hali inayompa kocha Hans Pluijm na benchi lake la ufundi wigo mpana wa kupanga kikosi kulingana na mahitaji.

Yanga inashika nafasi ya tatu ikiwa na alama 15 huku ikiwa na mchezo mmoja mkononi dhidi ya JKT Ruvu baada ya kushuka dimbani mara nane.

Post a Comment

 
Top