BOIPLUS SPORTS BLOG

Zainabu Rajabu,Dar
UBORA wa safu ya ushambuliaji ya Simba hasa Ibrahim Ajib na Shiza Kichuya umewastua mabeki wa Mbeya City ambao sasa wameanza kupanga mbinu mpya za kuwadhibiti ili kupunguza kasi yao ya kutikisa nyavu.

Ajib na Kichuya wamekuwa tishio kwa timu nyingi za ligi kuu kwani wanapopata nafasi nzuri ya kufunga huwa hawakosei ambapo sasa wamechangia kwa kiasi kikubwa timu yao kuendelea kukaa kileleni ikiwa na pointi 17 na Jumatano Simba itakaribishwa kucheza na City kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.

Akizungumza na BOIPLUS beki mkongwe wa Mbeya City, Haruna Shamte alisema kuwa watapambana kuhakikisha hawapotezi mechi hiyo na kuwabana vilivyo wasumbufu hao ili wasipenye ngome yao na kuleta madhara.

“Uwezo wetu kwasasa ni mzuri na tumedhamiria kupata pointi tatu toka Simba ingawa tunafahamu kuwa hata wao wanazihitaji pointi hizo lakini tutaweka ulinzi wa kutosha kuwazuia nyota wao hao ambao ndiyo tegemeo kwa timu hiyo ili wasipite," alisema Shamte huku akisisitiza kuwa Kichuya na Ajib hawawezi kupenya mbele ya Sankhani Mkandawile ,Hassan Mwasapile na Rajabu Zahir.

Mbeya City imefikisha pointi 12 na kushika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi hiyo na ikimaliza tu mechi hiyo itaanza safari ya kuja mkoani Pwani kucheza na JKT Ruvu uwanja wa Mabatini.

Post a Comment

 
Top