BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
BAO la kusawazisha la dakika za majeruhi la mpira wa kona wa moja kwa moja lililofungwa na winga Shiza Kichuya dhidi Yanga kwenye mchezo uliofanyika Oktoba mosi Uwanja wa Taifa  limemuweka jukwaani kipa Ally Mustapha 'Barthez' baada ya wadau wengi kupaza sauti kuwa alikosa umakini.

Barthez alishindwa kujipanga vizuri langoni mwake katika mtanange huo ambao mabingwa hao walikuwa wakiamini kuwa wataondoka na alama zote tatu lakini bao hilo la Kichuya liliharibu shughuli nzima kiasi cha mashabiki kuanza kumtupia kipa huyo maneno ya kucheza chini ya kiwango.

Kwa kuonesha kuwa benchi la ufundi la Yanga chini ya Kocha Hans van Pluijm halikuridhishwa na kitendo hicho katika mchezo wa leo dhidi ya Mtibwa Sugar utakaopigwa kwenye uwanja wa Uhuru kipa huyo hatakuwepo kabisa hata benchi baada ya kuanzishwa Deogratius Munishi Dida' huku benchi akiwepo Beno Kakolanya.

Mabadiliko mengine ndani ya kikosi cha Yanga kinachoanza leo ni mshambuliaji tegemeo Donald Ngoma kuanzia benchi huku Obrey Chirwa akianza baada ya kushindwa kufunga goli lolote hadi sasa tangu ajiunge na mabingwa hao mwezi Juni.

Kiungo Saidi Makapu ameanza katika kikosi cha kwanza baada ya kukosekana kwa muda mrefu na amechukua nafasi ya Mbuyu Twite ambaye leo hii yuko benchi.

Beki Vicent Bossou hatakuwepo kwenye mchezo kufuatia kuchelewa kuripoti kambini baada ya majukumu ya timu yake ya Taifa ya Togo kwenye mechi za kufuzu kombe la dunia. Andrew Vicent Dante' atacheza nafasi hiyo sambamba na Kelvin Yondani.

Post a Comment

 
Top