BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Mbeya
SIMBA imepata pointi tatu muhimu za ugenini huku nyota wao Shiza Kichuya na Ibrahim Ajib wakiwa ndiyo walioilaza Mbeya City na njaa ingawa Kichuya alishindwa kumalizia mechi hiyo baada ya kugongana na wachezaji wa City wakati wa kuwania mpira.

Mbali na kujikusanyia pointi  19 zilizowafanya waendelee kukaa kileleni, kocha wa Simba Joseph Omog alionekana kumwamini sana winga wake Kichuya na kumpa nafasi ya kupiga mipira yote ya kona ambapo Simba ilipata kona sita lakini Kichuya alipiga tano kabla ya kutolewa nje akishindwa kuendelea na mchezo baada ya kuumia.

Kona ya sita ya Simba ilimaliziwa na Janvier Bokungu ingawa zote hazikuzaa matunda kutokana na umakini wa safu ya ulinzi ya Mbeya City ambao walipata kona nne na hawakuzitendea haki.

Mechi hiyo imechezwa uwanja wa Sokoine jijini Mbeya na imemalizika kwa Simba kupata ushindi wa bao 2-0. City wataanza safari alfajiri ya kesho kuelekea mabatini kuwafuata Ruvu Shooting.

Ajib ndiye aliyeanza kutikisa nyavu za wapinzani wao dakika ya tano tu tangu kuanza kwa mchezo huo akipiga mpira wa faulo uliotinga nyavuni moja kwa moja wakati Kichuya bao lake alilifunga dakika ya 33 akipokea pasi ndefu ya Jonas Mkude.

Pamoja na ushindi huo lakini Ajib na Fredrick Blagnon walikosa mabao dakika za mwanzo tu baada ya kipa wa City, Owen Chauma kuokoa, Ajib alikosa bao dakika ya kwanza huku Blagnon yeye akishindwa kutikisa nyavu dakika ya pili.

Dakika ya 12 Simba walipata penati baada ya Blagnon kufanyiwa madhambi na Rajab Zahiri, penalti hiyo ilipigwa na Blagnon lakini ilikuwa nyepesi hivyo kudakwa kirahisi  na Chauma.

Kipindi cha kwanza City walifanya shambulizi moja pekee la Omary Ramadhan katika dakika ya 26 lakini shambulizi hilo halikuwa na madhara baada ya beki Method Mwanjali kuokoa hatari hiyo huku Ajib akijibu shambulizi hilo dakika 27 kwa kupiga shuti la mbali lililogonga mwamba.

Ajib alionekana kuwang'ang'ania Mbeya City kwani dakika ya 30 alikosa bao lingine baada ya mpira wake kutoka nje kidogo ya goli la City huku Blagnon naye akikosa bao dakika 42 wakati wa piga nikupige langoni mwa City ila shuti lake lilidakwa na mlinda mlango wa Wagonga nyundo hao.

Omog alifanya mabadiliko ambapo aliwatoa Blagnon, Ajib na Kichuya aliyeshindwa kuendelea na mchezo baada ya kuumia nafasi zao zilichukuliwa na Ame Ally, Said Ndemla na Mohamed Ibrahim huku Kinah Phiri akimtoa Kabanda na Ditrman Nchimbi nafasi zao zikichukuliwa na Hemed Murutabose pamoja na Salvatory Nkulula.

Dakika ya 72 Ndemla alipiga shuti kali akiwa umbali wa mita 20 toka langoni ambalo lilimpita kipa wa City katika ya miguu yake lakini aliokoa huku Kazimoto naye akipiga shuti ambalo lilisababisha  kona iliyopigwa na Bokungu lakini haikuzaa matunda.

Kocha wa City, Phiri anapaswa kufanya marekebisho hasa safu yake ya ushambuliaji ambayo inaonekana kuwa butu na kukosa kabisa kufika langoni mwa wapinzani wao hata wakipata nafasi wanashindwa kumalizia.

Post a Comment

 
Top