BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
HII ni mara ya pili sasa kwa Simba kukombolewa dakika za lala salama, awali winga wao Shiza Kichuya aliisawazishia bao dakika ya 87 wakati tayari Yanga wakiwa wanaoongoza na jana Mzamiru Yassin naye kafunga bao pekee dakika hiyo hiyo ya 87 dhidi ya Mbao FC ya jijini Mwanza.

Nyota hao wote wamesajiliwa msimu huu wakitokea Mtibwa Sugar tena kwa dau la kawaida tu ila mchango wao ndani ya Simba umekuwa mkubwa kutokana na jinsi wanavyopambana kuipatia Simba matokeo mazuri. Kama asingekuwa Mzamiru basi jana Simba ingetoka sare kutokana na umahiri wa kikosi cha Mbao hasa walipocheza soka la kutofunguka na kufanikiwa kuwanyima nafasi washambuliaji wa Wekundu huo.

Mechi ya Simba na Yanga ilichezwa uwanja wa Taifa huku bao la Kichuya likonekana kuwatuliza hasira zilizokuwa zimewapanda mashabiki wa Simba hasa mwamuzi Martin Saanya alipompa kadi nyekundu Jonas Mkude na kukubali bao la Amissi Tambwe lililodaiwa kuwa alifunga baada ya kumiliki mpira kwa mkono.

Mzamiru yeye jana aliibuka shujaa kwenye dakika hizo baada ya kupokea pasi nzuri ya Fredrick Blagnon aliyechukuwa nafasi ya Laudit Mavugo huku Mzamiru akisema siri kubwa ya nyota hao kufunga mabao ni kuusoma kwanza mchezo mzima ulivyo.

"Mbao si timu ya kuibeza eti kwasababu tu ndiyo imepanda daraja, kiwango chao sasa hivi kimepanda na wanaonekana kila mechi wanayocheza wanabadilika, hivyo kwa mechi kama hiyo unatakiwa kuwa makini kusoma mchezo, hicho ndicho kikubwa kinachotusaidia, pia ukiwa kwenye nafasi nzuri unapaswa kujaribu kufanya jambo iwe kwa mafanikio ama kwa vyovyote itakavyokuwa," alisema Mzamiru.

Post a Comment

 
Top