BOIPLUS SPORTS BLOG

Karim Boimanda
TIMU ya Kilimanjaro FC iliyoundwa na watanzania waishio nchini Sweden leo imefanikiwa kupanda hadi daraja la sita baada ya kulazimisha sare ya bao 1-1 dhidi ya wapinzani wao wakubwa Solna FC kwenye mchezo wa mwisho wa makundi ligi daraja la saba.

Kilimanjaro wanaoizidi Solna pointi moja tu walikuwa wanahitaji sare au ushindi wa aina yoyote ili kupanda daraja huku wapinzani wao wakiingia uwanjani kwa lengo la kupata pointi tatu.

Mchawi wa mabao wa zamani wa Simba SC ya Dar es Salaam, Athumani Machupa ndiye aliyepeleka kilio kwa 'waswidishi' hao baada ya kutupia bao pekee la Kilimanjaro katika mchezo huo uliokuwa kama fainali.

'Wakali' wa Tanzania walioipandisha timu hiyo ni pamoja na kiungo 'Maestro' wa zamani wa wekundu wa Msimbazi Shekhan Rashid, Machupa, William John ambaye aliwahi kutisha na Simba pia, Credo Mwaipopo aliyetisha akiwa Yanga, Khamis Abui aliyekuwa nahodha wa Moro United (2001) na vijana wengine kadhaa.
Kiungo wa Kilimanjaro FC, Shekhan Rashid akifurahi na familia yake baada ya kumalizika kwa mechi hiyo

Timu hiyo yenye nyota wengine kutoka nchi za Kenya na Gambia imemaliza michuano hiyo ikiwa na pointi 41 na itashiriki ligi daraja la sita inayotarajiwa kuanza mwezi Aprili na kumalizika Oktoba mwakani.

Lengo la kuanzishwa kwa timu hiyo ni kuifikisha daraja la pili ambako huchezwa soka la kulipwa hatua ambayo itawawezesha kuita vijana wa kitanzania kwenda kuonyesha vipaji vyao ili waweze kununuliwa na klabu kubwa barani Ulaya.

BOIPLUS Blogspot inawapongeza viongozi, makocha na wachezaji wa Kilimanjaro FC kwa hatua hiyo kubwa waliyofikia.

Post a Comment

 
Top