BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
SIMBA sasa inazidi kuwa imara baada ya kuwasili kwa ITC ya kiungo wao Mussa Ndusha ambayo tayari imepokelewa na Shirikisho la Soka nchini (TFF) hivyo uwepo wa kiungo huyo utaongeza pia ushindani kwenye nafasi hiyo.

Tangu kiungo huyo Mkongomani asajiliwe hajawahi kucheza mechi hata moja ya ligi kuu huku uongozi wa Simba ukipambana kuhakikisha ITC hiyo inapatikana ambapo imetolewa moja kwa moja na FIFA hivyo Kocha Joseph Omog atakuwa huru kumtumia sasa.

Uongozi wa Simba ulikabidhi jukumu la ufuatiliaji kwa ukaribu zaidi wa ITC hiyo kwa meneja wa klabu anayeshughulikia usajili huo wa FIFA kwa njia ya mtandao TMS, Collins Frisch 

Ndusha ambaye ameichezea Simba mechi mbili pekee za kirafiki dhidi ya AFC Leopard na kushinda bao 4-0 na mechi nyingine ni ile ya sare ya bao moja dhidi ya URA ataingia vitani na viungo Jonas Mkude, Mzamiru Yassin, Mohamed Ibrahim, Said Ndemla, Mwinyi Kazimoto na Awadh Juma ambaye ni kama amepotea.

Makamu wa Rais wa Simba, Geofrey Nyange Kaburu amethibitisha hilo na kuushukuru uongozi wa klabu yao kuhakikisha hilo linakamilika kwa haraka kwani mchezaji huyo alisaini mkataba wa miaka miwili baada ya kufuzu majaribio.

"Ndusha alisaini mkataba wa miaka miwili Agosti Mosi baada ya kufaulu majaribio yeye na mwenzake Janvier Bokungu ambaye ana mkataba wa miezi sita, hivyo ni kweli ITC yake imewasili sasa ni ruhusa kumtumia," alisema Kaburu.

Kwa upande wa Bokungu yeye atasuburi taarifa ya kocha Omog kama atakuwa ameridhishwa na kiwango chake katika mechi alizocheza na ndipo mkataba wake utajadiliwa upya kama ni kumwongeza ama kuachana naye.

Post a Comment

 
Top