BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
PAMOJA na kukubali kipigo cha bao 2-0 kutoka kwa African Lyon lakini malengo ya kocha wa Mbeya City ya kumaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom akiwa amekusanya pointi 20 bado hayajaharibika, mechi hiyo imechezwa uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Mabao ya Lyon yamefungwa na mshambuliaji wao Titto Okello dakika ya 55 kwa shuti kali akimalizia mpira uliokolewa na walinzi wa MCC huku bao la pili likifungwa dakika ya 90 na Rehabi Kipingu hivyo matokeo hayo yamezifanya timu zote mbili ziwe na pointi 13 wakitofautiana kwa idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Kwa mahesabu ya Phiri, City bado ina nafasi ya kukusanya pointi 12 katika mechi zake tatu zilizobaki za mzunguko wa kwanza ambapo sasa watakwenda kucheza na Majimaji mjini Songea, watarudi nyumbani kuwakaribisha Yanga na baadaye kurudi Manungu kucheza na Mtibwa Sugar.

Endapo City watafanikiwa kushinda mechi zao tatu zilizobaki za mzunguko huu wa kwanza basi watakusanya pointi 12 ambazo zitawapa pointi 25 ambazo ni zaidi ya 20 alizojiwekea Phiri katika malengo yake lakini wakipoteza ama kutoka sare zote basi malengo yake hayatatimia.

Akizungumza na BOIPLUS, Phiri alisema kuwa sasa hivi anaangalia mechi zijazo jinsi ya kupata ushindi ingawa aliamini kwamba hata mechi hii wangeshinda.

"Tumepoteza mchezo na wenzetu wamefanikiwa kupata pointi tatu, ila nataka kumaliza huu mzunguko nikiwa na pointi 20 na itawezekana, tumefanya makosa wenzetu wametumia makosa yetu.

"Lakini pia ratiba ya ligi muda mwingine inawachosha sana wachezaji maana tunazunguka sana na hatupati muda wa kupumzika hivyo ni lazima tupambane kuzipata pointi hizo," alisema Phiri.

City ambayo imetokea Mtwara kucheza na Ndanda Fc na kuambulia sare ya bao moja itaondoka kesho kuelelekea mjini Songea tayari kwa mechi yao na Majimaji ambao pia sasa wanapambana kupata ushindi kutokana na kufanya vibaya mechi zilizopita.

Post a Comment

 
Top