BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
LIGI ya Taifa ya wanawake inatarajiwa kuanza Novemba mosi kwa kushirikisha timu 12 kutoka mikoa mbali mbali nchini ambayo itaoneshwa moja kwa moja na kituo cha Luninga cha Azam TV.

Ligi hiyo ambayo inafanyika kwa mara ya kwanza nchini itakuwa na makundi mawili yenye timu sita kila moja na washindi watatu wa kila kundi watawekwa kwenye kituo kimoja ambacho kitatangazwa baadae ndipo atakapopatikana mshindi wa jumla.

Ligi hiyo ambayo haitaingiliana kiratiba na ligi ya Vodacom na ile ya Daraja la kwanza itachezwa kwenye viwanja vifuatazo; Uwanja wa Uhuru, Karume, Nangwanda Sijaona, CCM Kirumba, pamoja na CCM Mkwakwani.

Kamati ya maendeleo ya soka la Wanawake itakutana siku ya Jumamosi Oktoba 22 kupitia mapingamizi ya wachezaji waliowekewa kutoka kwenye timu husika ili kuondoa malalamiko ambayo yatakuja kujitokeza siku za usoni.

Afisa Habari wa Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) Alfred Lucas amewataka wadau mbali mbali kujitokeza kudhamini ligi hiyo kwakua kuna fursa ya kujitangaza kama kwenye ligi kuu ya Vodacom na ile ya Daraja la kwanza.

"Tunawaomba wadau wajitokeze kudhamini ligi hii ili kuongeza ushindani kwani mpira kwa sasa umekuwa ajira na kila mmoja anapenda kuona analipwa kulingana na jasho lake," alisema Lucas.

Katika ligi hiyo timu zinaruhusiwa kusajili wachezaji saba wa kigeni kama ilivyo kwa ligi kuu ya Vodacom.

Makundi ya timu hizo 12

Kundi A
Viva Queen - Mtwara
Mburahati Queen - Dar es Salaam
Fair play FC - Tanga
Evergreen Queen - Dar es Salaam
Mlandizi Queen - Pwani
JKT Queen - Dar es Salaam

Kundi B
Marsh Academy - Mwanza
Baobab Queen - Dodoma
Majengo Women FC - Singida
Sisterz FC - Kigoma
Kagera Queen -Kagera
Panama FC - Iringa

Post a Comment

 
Top