BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
LIGI ya Taifa ya Wanawake itazinduliwa Novemba mosi mkoani Dodoma kwa mchezo kati ya timu ya Baobab Queen ya mkoani humo dhidi ya Victoria mchezo utakaochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri.

Ligi hiyo itashirikisha timu 12 kutoka mikoa mbali mbali nchini ambayo michezo yake itaonyeshwa moja kwa moja na kituo cha Luninga cha Azam TV ambao ndiyo wadhamini wakuu huku pesa za awali za maandalizi zikiwa zimeshapelekwa kwenye mikoa inayotoka timu shiriki.

Msemaji wa Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) Alfred Lucas alisema kuwa rufaa zote zilizokatwa kwa baadhi ya wachezaji zimeshindwa baada ya wakataji kushindwa kupeleka vielelezo sahihi na hivyo wanandinga hao wataruhusiwa kucheza katika timu zilizowasajili.

Lucas alisema kuwa katika ligi hiyo waamuzi Wanawake ndiyo watachezesha mechi hizo ili kuongeza chachu huku marefaa wa kati ambao wanatambuliwa na FIFA wapo wanne hadi sasa hali inayoonesha kuwa wataweza kumudu kashkashi hizo.

"Ligi itazinduliwa Novemba mosi mkoani Dodoma na ndiyo siku ambayo vikao vya Bunge vitaanza na tunatarajia Waheshimiwa Wabunge wengi kushuhudia ufunguzi huo huku Wanawake wakipewa kipaumbele katika jambo hilo," alisema Lucas.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Michezo cha Azam TV Baruhan Muhuza alisema wameamua kudhamini kwa kuonesha moja kwa moja michuano hiyo kwa ajili ya kuwavutia watu wengine kujitokeza kusaidia kwa ajili ya kuinua soka la Wanawake.

Naye Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Wanawake Sebastian Mkoma alisema atatumia mashindano hayo kuzunguka na benchi lake la ufundi kwa ajili ya kuchagua nyota watakaojiunga na Twiga Stars ambao watakuwa bora zaidi.

Post a Comment

 
Top