BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
IMEELEZWA kuwa kocha George Lwandamina raia wa Zambia ambaye tayari yupo nchini na anatajwa kuwa atasaini mkataba wa miaka miwili na Yanga huwa anataka mambo matatu makubwa kutoka kwa nyota wake ambayo ni nidhamu, kujituma na suala la kufunga ambalo humpa mchezaji yoyote atakayekuwa kwenye nafasi ya nzuri.

Kocha mkuu huyo wa Zesco ambao ni Mabingwa wa Ligi Kuu Zambia aliwasili nchini jana kwa siri kubwa na suala lake la mkataba linafanywa kwa usiri mkubwa mno huku hatima ya Hans Pluijm bado ikiwa haijajulikana hadi sasa kwani hajapewa taarifa yoyote ya mabadiliko kwenye benchi lake la ufundi.

Straika wa Zesco, Juma Luizio ameiambia BOIPLUS kuwa endapo Yanga watafanikisha dili hilo basi watakuwa wamelamba dume na kuwatahadharisha wachezaji wa Yanga kufuata yale ambayo kocha huyo anatayataka kutoka kwao, nidhamu, kujituma na kufunga mabao.

"Huyu kocha hana tatizo na mtu, ni kocha mzuri na anauwezo wa kuishi na mtu yeyote, huwa hamtengi mchezaji yeyote na anataka timu ifunge mabao mengi, hupendelea kucheza soka la kisasa kwani anapenda kutumia mifumo ya mafanikio. Kikubwa ambacho wachezaji wanatakiwa kuzingatia zaidi na kufanyia kazi ni nidhamu na kujituma maana hilo huwa anasisitiza sana.
Juma Luizio (kushoto)
"Ukichelewa mazoezini, muda wa kula au kwenda kula ukiwa na simu mkononi unakatwa pesa ambapo makato ya chini kabisa ni sh. 25,000 ya huko Tanzania," alisema Luizio.

Mabadiliko hayo yanafanyika huku Yanga ikiwa imecheza mechi 10 za Ligi Kuu na kukusanya pointi 21 ikishika nafasi ya pili kwenye msimamo lakini mabadiliko hayo pia yanaweza kuwa mazuri ama mabaya kwa Yanga kwani inaelezwa kuwa kitaalamu kubadilisha kocha katikati ya msimu kunaiporomosha timu zaidi.

Lakini kitu ambacho kinaweza kuwasaidia Yanga kubaki kwenye kiwango chao kama Mzambia huyo ataanza kazi basi ni mifumo yake anayopendelea kuitumia mara kwa mara. Lwandamina hupenda kutumia mifumo miwili zaidi 4-2-3-1 na 4-4-2 ambayo pia hutumiwa na Pluijm.

Pluijm yupo na kikosi sasa ambacho kinajiandaa na mechi dhidi ya JKT Ruvu itakayochezwa keshokutwa Jumatano uwanja wa Uhuru, mechi hiyo ni ya kiporo kwa Pluijm, hivyo baada ya mechi hiyo lolote linaweza kutokea kwake.

Mabadiliko hayo yanatajwa kumgusa pia kocha msaidizi Juma Mwambusi, kocha wa makipa Juma Pondamali na Meneja Hafidh Salehe huku nafasi zao zikitajwa kuchukuliwa na kocha wa Taifa Stars, Boniface Mkwasa, kocha wa makipa anatajwa Manyika Peter huku huku meneja akipendekezwa mchezaji wao wa zamani Sekilojo Chambua.

Post a Comment

 
Top