BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma
MBUYU Twite ameweka historia baada ya kufunga bao kwa mpira wa kurusha ambao uliguswa na mlinda mlango Emanuel Mseja kabla haujatinga wavuni na kuisaidia timu yake ya Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Mbao FC kwenye Uwanja wa Uhuru. Hata hivyo Azam TV wamelitaja bao hilo kama la kujifunga.

Twite amekuwa na kawaida ya kurusha mipira inayotoka karibu na lango la wapinzani kutokana na nguvu alizonazo ambapo alifunga bao hilo dakika ya 54 katika mchezo ambao Kocha Hans Pluijm aliongoza benchi la ufundi tangu arejee baada ya kuandika barua ya kujiuzulu.

Vicent Bossou ndiye alikuwa wa kwanza kuwapatia bao mabingwa hao watetezi dakika ya 49 kwa kichwa baada ya kutokea piga ni kupige langoni mwa Mbao huku Wachezaji wake wakishindwa kujipanga vizuri.

Mbao waliweza kuwabana vizuri Yanga kipindi cha kwanza ambapo walicheza kwa kuelewana na mipango na kutoruhusu nyavu zao kuguswa kabla Mabingwa hao hawajawabadilikia dakika 45 za kipindi pili.Mshambuliaji Amissi Tambwe alifikisha idadi ya mabao saba hadi sasa kwenye msimamo wa wafungaji bao moja pungufu ya Shiza Kichuya baada ya kupokea pasi safi ya Haruna Niyonzima dakika ya 75 na kumchambua kipa Mseja.

Baada ya mabao hayo Yanga waliendelea kutandaza soka safi kwa kushambulia lango la Mbao lakini mabeki waliokuwa chini ya Asante Kwasi waliongeza umakini ili wasiendelee kupata dhahama zaidi.

Yanga iliwatoa Deus Kaseke, Obrey Chirwa na Hassan Kessi na kuwaingiza Juma Mahadhi, Thabani Kamusoko na Donald Ngoma. Mbao iliwapumzisha Hussein Sweddy na Venance Ludovic na kuwaingiza Frank Damas na Emmanuel Mvuyekure.

Yanga wamefikisha alama 27 wakiwa nafasi ya pili pointi tano nyuma ya vinara Simba ambao nao walishinda jana mabao 3-0 dhidi ya Mwadui FC.

Post a Comment

 
Top