BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
BAADA ya kushindwa kufuzu michuano ya AFCON U17 kwa kuchapwa bao 1-0 na Congo Brazaville jana, wachezaji wa timu ya Taifa ya Vijana (U17) 'Serengeti Boys' waliangua kilio uwanjani huku hali hiyo ikimgusa Rais wa TFF Jamal Malinzi aliyetangaza kuwapoza.

Serengeti walifanya jitihada kubwa ya kulinda ngome yao ili wasifungwe ambapo sare yoyote ingewawezesha kucheza fainali hizo ambazo zitafanyika mwakani nchini Madagascar lakini bao la jioni la Wakongomani hao lilifuta ndoto zao.

Baada ya mchezo huo Malinzi aliwapongeza vijana hao kwa kusema kuwa walipambana vya kutosha lakini bahati haikuwa upande wao ndiyo maana wakashindwa kufuzu michuano hiyo.

"Wamejitahidi sana, bahati tu ndio haikuwa upande wao. Timu itawasili nchini kesho Jumanne saa 3 usiku kwa ndege ya Rwanda Air ambapo keshokutwa mchana tutapata chakula cha pamoja na wachezaji hao ili kuendelea kuwapa hamasa kwa walichokifanya licha ya kushindwa kufuzu," alisema Malinzi.

Aidha Malinzi alisema watawatangaza vijana hao kuwa ndio Ngorongoro Heroes ya mwaka 2019 kabla ya kuwa 'Taifa Stars' mwaka 2021 huku viongozi wa Shirikisho hilo wakiwa wamepanga kuwatunza nyota hao ili wawe msaada kwa nchi siku zijazo.

"Ili adhma hiyo itimie ni lazima vijana hao wakuzwe katika maadili na nidhamu ya soka ili kuwachunga na kutojiingiza kwenye anasa za dunia ambazo zitaathiri viwango vyao na kuzipeperusha ndoto zao" alimaliza Malinzi.

Post a Comment

 
Top