BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
MWENYEKITI wa klabu ya Yanga Yusuph Manji amemtaka Katibu wa Baraza la Wazee Mzee Ibrahim Akilimali kuhudhuria kwenye mkutano mkuu wa dharura utakaofanyika Jumapili Oktoba 23 kama amelipia kadi yake ya uanachama kwa mujibu wa katiba ya Yanga.

Mzee Akilimali pamoja na wazee wenzake wa Baraza hilo walijitokeza hadharani mapema wiki hii kuupinga mkutano huo kwa madai kuwa umekiuka katiba ya Yanga na pia suala zima la ukodishwaji wa nembo ya timu hiyo ni batili kutokana na bodi ya udhamini iliyosaini mkataba na kampuni ya Yanga Yetu kuwa haipo kisheria kwavile ni ya mpito na haikusajiliwa RITA.

Manji alisema mbele ya Waandishi wa Habari kuwa wanachama wote wa klabu ya Yanga akiwemo Mzee Akilimali wanapaswa kuhudhuria kwenye mkutano huo utakaofanyika klabuni hapo kuanzia saa 3 asubuhi lakini lazima wawe wamelipia kadi zao za uanachama.

"Watakaoruhusiwa kushiriki mkutano huo ni wale tu waliolipia kadi zao za uanachama kwahiyo kama Mzee Akilimali amelipia basi aje mkutanoni atapewa nafasi ya kutoa maoni yake kuhusu mustakabali wa timu yetu kwa sababu tunahitaji mshikamano ndani ya Yanga," alisema Manji.

Kumekuwa na taarifa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii kuwa Katibu huyo hajalipia kadi yake kwa ziada ya miezi sita kitu ambacho ni kinyume na katiba ya klabu hiyo ambayo itamfanya kushindwa kushiriki kwenye mkutano huo.

Mzee Akilimali mwenyewe alisema mbele ya Waandishi wa Habari mapema wiki hii kuwa hatahudhuria mkutano huo kwavile umekiuka katiba ya klabu hiyo.

Post a Comment

 
Top