BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
WANACHAMA wa klabu ya Yanga wametakiwa kujitokeza kwa wingi kwenye mkutano mkuu wa dharura utakaofanyika Oktoba 23 Makao makuu ya klabu Jangwani jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujadili masuala mbali mbali likiwemo suala la ukodishwaji.

Mwenyekiti wa Klabu hiyo Yusuph Manji amewaambia waandishi wa Habari kuwa mkutano huo utakuwa wa wazi na kila mwanachama atapewa nafasi ya kutoa maoni yake juu ya suala zima la uendeshwaji kwa ajili ya maendeleo ya Yanga.

Manji alisema badala ya wanachama kukimbilia kwenye vyombo vya Habari kuongea kuhusu masuala ya klabu wanatakiwa kujitokeza kwa wingi kwenye mkutano huo ili kuchangia kwa manufaa ya Yanga.

"Mkutano utakuwa huru na wa haki kila mwanachama ambaye amelipia kadi yake atapewa nafasi ya kutoa duku duku lake kabla ya makubaliano kufikiwa," alisema Manji.

Manji alisema baada ya makubaliano hayo kufanyika Uwanja wa mazoezi utaanza kujengwa ndani ya siku 90 katika eneo la Gezaulole lililopo Kigamboni kwa mujibu wa mkataba uliosainiwa na kampuni ya Yanga.

Aidha Manji alisema kuhusu suala la kusainiwa kwa mkataba na bodi ya wadhamini dhidi ya kampuni ya Yanga Yetu kila kitu kitajadiliwa kwenye mkutano huo ambapo wanachama wametakiwa kuwahi mapema huku ulinzi ukiwa ni uhakika.

Post a Comment

 
Top