BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
IKIWA imebaki wiki moja kuelekea mkutano mkuu wa dharura wa klabu ya Yanga utakaofanyika Jumapili ijayo Oktoba 23 wanachama wa klabu hiyo wamewataka watu wasio itakia mema klabu hiyo wakae mbali nayo.

Kundi la wanachama wa klabu hiyo toka kwenye mitandao ya kijamii Yanga Online Fans 'YON' limewataka wanachama kuwapuuza wale wasiotakia mema na kujitokeza kwa wingi kwenye mkutano huo utakaofanyika Jumapili ijayo kwa ajili ya kujadiliana masuala mbali mbali likiwemo suala la ukodishwaji.

Mwenyekiti wa kundi hilo Alhaji Saidi Side amewaambia waandishi wa Habari kuwa kuna njama zinafanywa na watu wasiopenda maendeleo ya Yanga kwa ajili ya kuvunja mkutano huo ili kurudisha nyuma harakati zao lakini wanatakiwa wawapuuze watu hao wasiwavuruge.


"Kuna watu wanashindwa kujadili hoja za msingi ndani ya klabu wanazungumza mambo binafsi na kama wanaona mkataba walioingia na kampuni ya Yanga Yetu sio mzuri wajitokeze Oktoba 23 kujadili kwa pamoja na sio kuzungumza kwenye mitandao kwa ajili ya kupandikiza chuki," alisema Side.

Kwa upande wake Mjumbe wa kundi hilo Kara Remtulah alisema wanachama wanahitaji furaha ambayo itatokana na kuwa na kikosi bora kutokana na uwekezaji mkubwa ambao Mwenyekiti Yusuph Manji anataka kufanya lakini watu wachache wenye maslahi yao binafsi wanapingana na jitihada hizo.

"Sisi wanachama tunahitaji furaha pekee ndani ya Yanga tukichukua ubingwa tunashangilia na uwekezaji kwenye klabu yoyote duniani hauepukiki kwahiyo hao wanaopinga hawana nia njema na Yanga," alisema Remtulah.

Wiki moja na nusu iliyopita uongozi wa timu hiyo ulitoa nakala ya mkataba uliosainiwa kwa ajili ya kuikodisha nembo ya klabu hiyo ambao umepokewa kwa hisia tofauti na wadau mbali mbali ambapo Baraza la Michezo Tanzania (BMT) pamoja na Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) wamesema hautambui mkataba huo huku wanachama wengine pia wakiupinga.

Post a Comment

 
Top