BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
 Francis Cheka kushoto akiwa na Thomas Mashali enzi za uhai wake

BONDIA Thomas Mashali amefariki dunia usiku wa kuamkia leo na kuacha pengo kubwa kwenye tasnia ya michezo huku pigo kubwa likiwa kwa mabondia wenzake ambao wameelezea hisia zao tofauti huku wengine tayari walimuweka kwenye ratiba za mapambano yao kwa mwaka huu.

Mashali aliyekuwa akipigana katika uzito wa 'Super Middle' kilo 76.6 alikutwa na mauti hayo akipelekwa hospitali ya Muhimbili baada ya hali yake kuwa mbaya zaidi alipopelekwa hospitali ya Palestina iliyopo Sinza akiwa amepigwa kichwani na kudaiwa kichwa kilipasuka na ubongo kutoka nje.

Mashali alipatwa na mkasa huo maeneo ya Kimara Bonyokwa huku Jeshi la Polisi Kanda ya Kinondoni, kupitia RPC Suzana Kaganda alisema walipata taarifa na kufika eneo la tukio ambapo walimchukuwa Mashali na kumkimbiza hospitali ambako mauti ilimkuta.

Suzana alisema awali kesi ambayo ilifunguliwa ni kesi ya mashambulizi na baada ya kifo kutokea kesi hiyo itageuzwa kuwa kesi ya mauaji ingawa bado watuhumiwa hawajapatikana na upelelezi unaendelea ambapo watatoa taarifa zaidi upelelezi ukikamilika.

Miongoni mwa mabondia ambao wameonyesha hisia zao ni Fransis Cheka aliyesema kuwa, "Ni kifo cha ghafla sana, kinaumiza kutokana na jinsi tunavyosimuliwa, wengi hatufahamu chanzo ila inauma, nilitakiwa kupanda naye ulingoni mwezi ujao (Novemba 26) katika pambano la kirafiki huku Morogoro ila haitakuwa tena kutokana na mauti iliyomkuta ndugu yetu.

"Nimewahi kupigana naye mara mbili na mara zote amenipiga, hivyo Mashali alikuwa bondia mzuri na ameacha pengo kubwa kwenye fani yetu, Mungu ampumzishe mahali pema peponi," alisema Cheka.

Mada Maugo kushoto akiwa na Mashali enzi za uhai wake

Kwa upande wa Mada Maugo alisema kuwa; "Taarifa zake nimezipata alfajiri ya leo, sikuamini kwa kweli kwani jana (Jumapili) tumezungumza na tuliahidiana kukutana leo (Jumatatu) ili tupange juu ya pambano la Desemba 25 ambalo tulitaka kupigana kuwania ubingwa wa WBF au IBF raundi 12 na uzito wa 'Super Middle'.

"Nilichagua kucheza na Mashali kwani ni miongoni mwa mabondia wazuri ambao nawakubali, ukipigana naye ujue kwamba unapigana na bondia mwenye uwezo mkubwa," alisema Maugo.

Baba mzazi wa Mashali, mzee Christopher Malifedha Mashali alisema kuwa; "Kuna vijana wanne walikuja kunigongea kwa fujo usiku wa saa 8.30 hivi, sikufungua mlango nilifungua pazia, niliwaomba mawasiliano yao ya simu waligoma kunipa kwa madai kuwa hawana simu, hata wakija hapa siwezi kuwakumbuka maana walionyesha kuwa na hofu na haraka.

"Hao ndiyo waliniambia Mashali kapigwa kichwa na ubongo umetoka nje na kwamba yupo hospitali Palestina niliwapigia simu wanangu ambao walikwenda pale ila walikuwa wameishampeleka Muhimbili na huko wakakuta amefariki. Hivyo tunasubiri taarifa ya polisi ili tujue chanzo cha kifo chake.

"Mara ya mwisho nimezungumza na mwanangu saa 11.24 jioni jana, nilimuuliza kama amempigia simu Promota Sadick Kinyogoli aliyetaka kumpa kazi, alinijibu kwa ujumbe mfupi kwamba 'bado nipo kwenye kikao nitakwambia baba' hayo ndiyo mawasiliano yangu ya mwisho na Mashali," alisema mzee Mashali.

Msiba wa Mashali upo nyumbani kwa baba yake Tandale ambapo mazishi yanatarajiwa kufanyika kati ya jijini Dar es Salaam ama nyumbani kwao Songwe na hiyo itajulikana baada ya familia kukaa na kuamua. Mashali ameacha watoto watano ambao wote ni wa kike, Rose, Rachel, Lilian, Lidiah na Jacqline.

Post a Comment

 
Top