BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
MSHAMBULIAJI wa zamani wa Simba, Emmanuel Gabriel 'Batgoal' ni kama vile amempa dongo nyota mwenzake Musa Mgosi kuwa hakupenda kustaafu ila amestaafishwa kwa kuzidiwa kete na vijana huku akimsihi Laudit Mavugo kuwa yasimkute kama ya Mgosi kucheza mechi 20 bila kufunga bao hata moja.

Hivi karibuni Mgosi alitangaza kustaafu soka na sasa ni meneja wa timu hiyo lakini Batgoal amekuwa na mtazamo tofauti kwamba endapo bilionea Mohamed Dewji 'Mo' akiichukuwa timu hiyo basi nafasi ya Mgosi ndani ya Simba itakuwa imeishia hapo na kumshauri kuwa aende akatafute timu ya kucheza umri bado unamruhusu.


Emmanuel Gabriel

Batgoal aliyeichezea Simba na Taifa Stars kwa mafanikio makubwa alisema kuwa endapo Mavugo ataikubali hali ya kushindwa kufunga ndani ya Simba basi mahali hapo hapatakuwa pa kwake na kuendelea kumpa mfano kupitia Mgosi aliyesema hakuwa mchezaji wa kustaafu sasa hivi.

"Mgosi kastaafishwa na vijana, alijikubali kuwa ameshindwa ndio maana akatoa uamuzi huo ambao binafsi naona haukuwa sahihi, unajua ukijiona tu umeshindwa ushindani nenda kacheze timu nyingine, Mgosi angerudi hata Mtibwa Sugar kuna wachezaji wenye umri mkubwa kuliko Mgosi ila wanacheza.


"Nasema hivi huyo Mgosi sasa hivi anafurahia maisha ya hapo Simba ila Mo akiingia huo ndiyo utakuwa mwisho wake na mkataba utakuwa umemalizika atakwenda kusaka timu. sidhani Mo kama atahitaji benchi la ufundi lenye watu wasiosomea fani husika kwa kiwango cha juu, atakwenda kucheza tu, amwangalie mwenzake Nico Nyagawa mkataba ulipokwisha aliondolewa," alisema Batgal.

Akifafanua juu ya Mavugo alisema kuwa; "Mavugo akiendelea hivyo basi naye anaweza kujikuta anafikisha mechi ya 20 akiwa na magoli hayo hayo manne, ni kweli kuna wakati mtu unashindwa kufunga ila usiikubali hali hiyo, alichokifanya Mavugo ni kujichukuliwa kuwa hakuna ushindani ndani ya Simba kwa jinsi alivyokuwa akizungumziwa midomoni mwa mashabiki, asipobadilika yatamkuta ya Mgosi."

Post a Comment

 
Top