BOIPLUS SPORTS BLOG

Akram Msangi, Shinyanga
PAMOJA na kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 ugenini dhidi ya Mwadui FC Kocha msaidizi wa timu ya Simba Jackson Mayanja hakuridhishwa na idadi hiyo ya mabao ambayo ingeongezeka zaidi endapo umakini ungeongezeka kwa wachezaji wake.

Simba walitengeneza nafasi nyingi kwenye mchezo huo ambapo kiungo Mzamiru Yassin alipoteza nafasi ya wazi kipindi cha kwanza huku Laudit Mavugo, Ame ally na Shiza Kichuya wakipoteza nafasi kadhaa.

Mayanja alisema kuwa anashukuru kwa ushindi huo mkubwa wa mabao matatu ugenini lakini amesikitishwa na wachezaji wake kushindwa kutumia nafasi walizotengeneza ambazo zingeweza kuzalisha mabao mengi zaidi na kuwaonya kutoridhika na matokeo kwakua kwenye ligi wakati mwingine Bingwa hupatikana kwa tofauti ya mabao.


"Tulitengeneza nafasi nyingi lakini tukatumia tatu zimetusaidia kutoka na pointi tatu ugenini na pia kitu cha kufurahisha katika kikosi kila mtu anaweza kufunga jambo ambalo ni faida kwa timu, lakini ni mbaya kupoteza nafasi nyingi," alisema Mayanja.

Kwa upande wake Kaimu Kocha Mkuu wa Mwadui Khalid Adam alisema kuwa Wachezaji wake walishindwa kuendana na kasi ya Simba na walifanya makosa mengi ambayo kama wapinzani wao wangekuwa makini zaidi wageibuka na mabao mengi.

Naye Meneja wa Simba Musa Mgosi alisema "Vijana wanaonekana wanaridhika mapema wanapopata mabao ni jukumu la mwalimu kulifanyia kazi ili tusije kupata shida huko mbeleni, ligi bado ni mbichi na kuna mechi zitakuwa ngumu kwetu kwahiyo lazima nafasi zinazopatikana zitumike kikamilifu".

Post a Comment

 
Top