BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally
STAND United leo wamekamatwa vibaya! Wamefunga safari mpaka Mbeya kuwavaa Maafande wa Magereza lakini kilichowakuta kinaweza kuwafurahisha Yanga na Azam kwani nao wamepigwa bao 2-1 kwenye uwanja wa Sokoine jijini humo.

Stand ikiwa nyumbani kwao Shinyanga ilifanikiwa kuwafunga Yanga na Azam huku wao wakienda Mbeya mara mbili na kuambulia pointi moja tu. Walicheza na Mbeya City walitoka sare na leo wamepoteza mchezo wao.

Baada ya kipigo hicho, Stand hawakukosa sababu kwani wamesema kwamba kufungwa kwao ni kama wamehujumiwa baada ya dakika 20 za mwisho mipira yote saba iliondolewa eneo la uwanja huo na kubakiwa na mpira mmoja tu, hivyo ukitoka nje basi utasubiriwa hadi ufuatwe.

Mbali na hilo, pia benchi la ufundi limelalamika kuwa mwamuzi wa mechi hiyo hakuwatendea haki katika baadhi ya maamuzi yake ingawa wamekubali kuwa mabao yote waliyofungwa na Prisons yamefungwa kiufundi.

Kocha Msaidizi wa Stand United, Athuman Bilali 'Billo' ameiambia BOIPLUS kuwa matokeo hayo hayawakatishi tamaa bali wataendelea kupambana ili wasishushwe kwenye nafasi hiyo ya pili japokuwa Yanga wanawapumulia kwani ushindi wao wa leo wa mabao 2-0 dhidi ya Toto umewafanya wafikishe pointi 18 wakati Stand wana pointi 20.

"Ni kweli tulizifunga timu kubwa kama Yanga na Azam, pia Simba tutawafunga ila kupiteza mechi ya leo si kwamba tumekata tamaa maana nimeona makosa ambapo bao la pili lilitokana na uzembe wa mabeki wangu ila kiukweli tumelazimishwa kufungwa.

"Ila pia hatujatendewa haki kuondolewa kwa mipira dakika za mwisho huko ni kutuhujumu. Tutapambana mechi zijazo ili tuendelee kubaki hapa juu tunafahamu kuwa Yanga wameshinda na isingekuwa rahisi Toto kuifunga Yanga hilo lipo wazi lakini tunasema tutabanana hapa hapa juu msimu huu," alisema Bilo

Mabao ya Prisons yalifungwa na wachezaji wao Lambert Sabianka na Salum huku bao la Stand United likifungwa na nahodha Jacob Masawe.

Post a Comment

 
Top