BOIPLUS SPORTS BLOG


Sheila Ally, Dar 
KIPA Juma Kaseja imedaiwa kuwa anataka alipwe kwanza pesa ya usajili ndani ya kikosi cha Mbeya City ndipo ataweza kuwatumikia na si vinginevyo lakini kocha wa timu hiyo, Kinnah Phiri sasa ameweka wazi kuwa hamuhitaji tena na ameanza kufikiria mbadala mpya wa kipa huyo kwenye usajili wa dirisha dogo.

Phiri raia wa Malawi alisema kuwa kitu pekee alichokigundua tangu afike Mbeya City ni jinsi wachezaji wa kitanzania wanavyoweka maslahi mbele pasipo kuangalia uwezo wa kucheza jambo ambalo amedai ndilo analolifanya pia kipa huyo mkongwe hapa nchini.

Aidha imeonekana kutokuwepo kwa mawasiliano ya wazi kati ya viongozi wa City na Phiri ambapo hivi karibuni uongozi ulisema kuwa Kaseja atajiunga na kikosi chao mara baada ya kurejea kwa Serengeti Boys kutokea Congo Brazaville kwani ruhusa yake ilikuwa inaendelea tangu wakati huo alipoombwa kuwafundisha makipa wa timu hiyo kwa muda huku Phiri akisema hana habari zozote kuhusu Kaseja.

Phiri alisema kuwa hivi sasa ataueleza wazi uongozi wake kwamba hamuhitaji tena kipa huyo kwani ameonekana kuwa msumbufu tangu msimu uliopita kwani aliwahi kuomba ruhusu ya kwenda kumhudumia mke wake alipojifungua ila alichelewa kurejea kikosini pasipo taarifa yoyote.

"Kama anahitaji kulipwa kwanza pesa si angekuja huku ili wamalizane, kiukweli nimechoshwa na hadithi hizo nitatafuta kipa mwingine wakati wa dirisha dogo, Kaseja pengine amepata mahali ambapo panamfaa na kumlipa vizuri na si hapa Mbeya City wenye uwezo mdogo kifedha, wachezaji hawana uchungu na mafanikio yao wakipata pesa hawajitumi.

"Lakini hili sio tatizo la Kaseja peke yake, wachezaji wengi wa Tanzania wanataka pesa kwanza na wakipewa baadhi yao hawachezi kwa kiwango kinachotakiwa hata hapa nimeona, hivyo kwa ushauri wangu wasingekuwa wanaweka pesa mbele wakati viwango vyao ni vya kawaida labda kama wana malengo ya kuishia hapa hapa Tanzania," alisema Phiri.

Post a Comment

 
Top