BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
MENEJA wa timu ya Majimaji ya mkoani Ruvuma Godfrey Mvula amejiuzulu nafasi hiyo kutokana na mwenendo mbovu wa 'Wanalizombe' hao na kuamua kujiweka pembeni kupisha watu wengine kwa ajili ya maendeleo ya timu hiyo.

Mvula aliyedumu na Wanalizombe hao kwa miaka 16 ameamua kukaa pembeni kama njia ya kujitathmini na kuwapisha watu wengine wenye mawazo mapya ambao wataweza kuitoa timu hiyo hapo ilipo na kuipeleka mbali zaidi kwa ajili ya maendeleo ya soka kwa mkoa mzima wa Ruvuma.

Mvula alitangaza azma yake hiyo ya kujiuzulu kwenye kipindi cha 'Michezo wiki hii' kinachorushwa kila siku ya Jumapili na kituo cha Radio cha Jogoo FM kilichopo mkoani humo huku Wanalizombe hao wakiwa bado hawako katika hali nzuri kutokana na kushika nafasi za mwisho mwisho kwenye msimamo wa ligi.

Mvula ambaye pia ni Katibu wa Chama cha Mpira Manispaa ya Ruvuma alisema ataendelea kuwa mwanachama wa klabu hiyo kwa kuendelea kuchangia michango mbali mbali ya kifedha na kimawazo katika kila atakapohitajika kwakua bado ana mapenzi ya dhati na Wanalizombe hao.

"Napenda kuwatangazia wapenzi na Wanachama wa Majimaji kuwa kuanzia leo nimejiuzulu nafasi ya Meneja wa timu hii ili kupisha watu wengine wenye uwezo wa kuivusha kutoka hapa ilipo na kuipeleka mbele zaidi. Nimekuwa na timu hii kwa miaka 16 sasa tangu nikiwa kijana wa miaka 25 hadi leo nina umri wa miaka 42 kwahiyo ni muda muafaka wa mimi kuwaachia wengine waendeleze hapa nilipoishia," alisema Mvula.

Majimaji inashika nafasi ya 14 katika msimamo wa ligi baada ya kujikusanyia alama 10 kwenye michezo 12 iliyoshuka dimbani ambapo katika mechi mbili za mwisho ilizocheza chini ya Kocha Kali Ongala iliibuka na ushindi.

Post a Comment

 
Top