BOIPLUS SPORTS BLOG

Akram Msangi, Dar
NAHODHA wa timu ya Simba Jonas Mkude amesikitishwa na mwamuzi Martin Saanya kwa kumtoa nje ya kwa kadi nyekundu katika mchezo dhidi ya Yanga Jumamosi iliyopita hali ya kuwa hajamfanyia kosa lolote.

Mkude alioneshwa kadi hiyo dakika ya 27 ya mchezo baada ya mshambuliaji Amisi Tambwe kufunga goli huku ikionekana ameushika mpira huo kabla ya kufunga  ndipo nahodha huyo alipomfuata mwamuzi kumlalamikia kabla ya kulimwa kadi nyekundu.

Mkude ameiambia BOIPLUS kuwa tukio la yeye kuoneshwa kadi ni moja ya mipango ya mwamuzi huyo ili kuidhoofisha timu lakini wachezaji wenzake walipambana na kusawazisha goli.

"Mimi nilimfuata mwamuzi kama nahodha wa timu kutokana na maamuzi mabovu, wala sikumsukuma ila nikashangaa ananipa kadi nyekundu, kiukweli imenisikitisha sana," alisema nahodha huyo.

Mkude alisema pia baada ya timu hizo kwenda mapumziko aliwahamasisha wachezaji wenzake waendelee kupambana na kusahau kuwa yeye hayupo uwanjani kitu ambacho walikifanya na kupelekea kutoa sare mchezo huo.

Aidha Mkude alisema "tatizo la waamuzi kuchukua pesa kwa ajili ya kuisaidia timu fulani ndiyo chanzo cha klabu za Tanzania kushindwa kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa na endapo wataendelea basi tutabaki hapa hapa tulipo."

Post a Comment

 
Top