BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imezuia mkutano mkuu wa dharura klabu ya Yanga uliopangwa kufanyika Jumapili Oktoba 23 kwenye uwanja wa Kaunda.

Zuio hilo la Mahakama limewekwa na aliyekuwa Mwanasheria wa klabu hiyo Frank Chacha kwa niaba ya wanachama wenzake ambaye ajira yake ilisitishwa mwezi Februari mwaka huu kutokana na sababu ambazo hazikuwekwa wazi.

Radio One kupitia kipindi chake cha 'Sports Leo' kimeripoti kuwa mkutano huo umezuiwa ikiwa imebakia siku moja kabla ya kufanyika kwa madai ya kukiukwa kwa katiba ya klabu hiyo kongwe iliyoanzishwa mwaka 1935.

Mapema leo Mwenyekiti wa klabu ya Yanga Yusuph Manji alifanya kikao na Waandishi wa Habari makao makuu ya timu hiyo akiwahamasisha wanachama kujitokeza kwa wingi kwenye mkutano huo kwa ajili ya mustakabali wa mabingwa hao wa kihistoria.

Katika mkutano huo kulikuwa na Ajenda 13 ambazo zingejadiliwa likiwemo suala la kukodishwa klabu hiyo na kampuni ya Yanga Yetu ambayo Manji anamiliki asilimia 99 huku akiwa ndiye Mwenyekiti wa klabu pia hali inayoonesha kuna mgongano wa kimaslahi.

Wiki mbili zilizopita uongozi wa Yanga ulitoa nakala ya mkataba uliosainiwa na bodi ya wadhamini wa klabu hiyo na Kampuni ya Yanga kuhusu ukodishwaji wa klabu hiyo hali iliyozua taharuki miongoni mwa wanachama hadi kufikia kupeleka suala mahakamani.

Post a Comment

 
Top