BOIPLUS SPORTS BLOG


Karim Boimanda
SIKU saba zimepita tangu Shiza Kichuya ‘ampe’ lawama kipa wa Yanga Ally Mustapha ‘Barthez’ kwa kumfunga bao kupitia mpira wa kona ya moja kwa moja lililoiwezesha Simba kupata sare ya bao 1-1 licha ya kucheza pungufu baada ya Jonas Mkude  kutolewa kwa kadi nyekundu.Bao hilo lilipeleka machungu makubwa kwa watoto wa Jangwani hali iliyopelekea baadhi ya mashabiki waanze kumtupia lawama kipa wao Barthez kuwa alifungwa bao la kizembe lililowanyima alama tatu muhimu.BOIPLUS imekukusanyia mabao matano ambayo wamefungwa makipa wazoefu duniani  na kuthibitisha kuwa  Kichuya hajafanya kitu kipya lakini pia Barthez si kipa wa kwanza kufungwa bao la aina ile.5. ROBERTO CARLOS vs Portuguesa FC

Tena akiwa na umri wa miaka 37, beki huyo wa kushoto aliyewahi kutamba na Real Madrid, akiitumikia Corinthians ya nchini kwao Brazil aliifungia timu yake bao la ‘kideoni’ kwa kona ya haraka haraka iliyokwenda moja kwa moja wavuni.

Kipa alisogea hatua moja mbele na Carlos akaona jambo hilo, alichokifanya yeye ni kupiga shuti la chini chini nyuma ya kipa wa Portuguesa na kuiandikia bao safi Corinthians.
4. THIERRY HENRY vs Columbus Crew

Hili ni bao kali la nyota wa zamani wa Arsenal alilowafunga Columbus Crew wakati akiichezea New York Red Bulls inayoshiriki ligi kuu nchini Marekani, MLS.

Unajua ilikuaje, Crew walikuwa wako mbele kwa bao 1-0 dakika ya saba ambapo Henry alipokea pasi ndefu na kuisawazishia Bulls katika dakika ya nane.  Baada ya dakika 90 kumalizika mwamuzi aliongeza dakika tisa, ilipotimu ya 92 tu Bulls wakapata kona iliyochongwa na Henry na kutinga moja kwa moja nyavuni huku kipa akidhani mpira huo utaambaa juu ya goli na kutoka nje.

3. DAVID BECKHAM vs Chicago Fire

Bado tukiwa ndani ya ligi kuu ya Marekani MLS, tunakutana na David Beckham nyota wa zamani wa Manchester United na Real Madrid.

Beckham akiichezea LA Galaxy aliipatia timu hiyo bao la ushindi katika dakika za ‘jioni’ kabisa baada ya kupiga kona iliyokatiza katikati ya mabeki wa Chicago Fire na kujaa nyavuni.
2. JOEY BARTON vs Borussia Monchengladbach

Baada ya kuipa kisogo ligi kuu ya Uingereza, Joey Barton alijitangaza vema mbele za mashabiki wa timu yake mpya ya Marseille inayoshiriki ligi kuu ya Ufaransa ‘Ligue 1’ kwa bao safi la kona ya moja kwa moja.


Walinzi  wa Monchengladbach walibaki wameduwaa tu wasiwe na la kufanya zaidi ya kumtizama kipa wao akichupa bila mafanikio. Bao hili linafanana kwa kiasi kikubwa na lile alilofungwa ‘Barthez’ na winga Kichuya juma lililopita, tofauti yake ni upande tu uliopigwa kona.
1.DIEGO FORLAN vs Fluminese

Likitajwa jina la straika huyu basi mashabiki wa Manchester United hupata kumbukumbu mbaya. Diego Forlan alisajiliwa na Sir Alex Ferguson kwa matumaini makubwa kuwa angeondoa ukame wa mabao klabuni hapo. Hali ilikuwa tofauti kabisa ambapo hakufanikiwa kuwafurahisha mashabiki wa Mashetani hao wekundu hadi anaondoka.


Hali ilianza kubadilika alipofika Atletico Madrid na hata katika fainali za kombe la dunia 2010 ambapo alionyesha uhai. Ilipofika 2012 Forlan alijiunga na vigogo wa Brazil, Internacional akitokea Inter Milan, na hiki hapa kwenye Video ndicho alichokifanya katika mchezo dhidi ya Fluminese.

Post a Comment

 
Top